Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 1 wa uvamizi wa Urusi Ukraine- Kilichojiri na kauli ya UN

Vituo vingi vya burudani vya manispaa kama mazoezi, mahakama za tenisi na mabwawa ya kuogelea vimeharibiwa vibaya au kuharibiwa huko Kyiv na Kharkiv.
© UNICEF/Mykola Synelnykov
Vituo vingi vya burudani vya manispaa kama mazoezi, mahakama za tenisi na mabwawa ya kuogelea vimeharibiwa vibaya au kuharibiwa huko Kyiv na Kharkiv.

Mwaka 1 wa uvamizi wa Urusi Ukraine- Kilichojiri na kauli ya UN

Amani na Usalama

Hii leo ni mwaka mmoja tangu Urusi ivamie Ukraine! Ndani ya mwaka mmoja wa uvamizi huo, zaidi ya watu 8,000,000 wamekimbia nchi hiyo, zaidi ya 5,000,000 ni wakimbizi wa ndani ilhali theluthi moja ya wananchi wote hawako kwenye makazi yao. Watu milioni 17.6 wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu ambapo zaidi ya milioni 16 wameshafikiwa na msaada muhimu.

Kilichotokea 24 Februari 2022  

Tarehe 24 mwezi Februari mwaka 2022 Mwakilishi wa kudumu wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Sergiy Kyslytsya akitangaza kwenye Baraza la Usalama akisema, Balozi wa shirikisho la Urusi dakika tatu zilizopita amethibitisha kuwa Rais wake ametangaza vita dhidi ya nchi  yangu.” 

Huo ulikuwa mwanzo wa uvamizi wa Urusi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye akizungumza na waandishi wa habari New York Marekani alisema, “Rais Putin!  kwa jina la utu wa kibinadamu rejesha majeshi yako Urusi. Tunashuhudia operesheni za jeshi la Urusi ndani ya ardhi huru ya Ukraine katika kiwango ambacho hakijashuhudiwa Ulaya katika miongo kadhaa. Ni kosa na ni kinyume cha Chata ya Umoja wa Mataifa.” 

Wakimbizi kutoka Ukraine wakiingia nchini Poland katika mpaka wa Medyka.
© UNHCR/Chris Melzer
Wakimbizi kutoka Ukraine wakiingia nchini Poland katika mpaka wa Medyka.

Maelfu ya raia wa Ukraine walianza kusaka usalama huku Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake na wadau nao wakisambaza misaada ya kibinadamu katika pande zote za mzozo. Katika kituo cha treni cha Lviv nchini Ukraine wengine waliweza kupata usafiri wa kukimbia kusaka usalama.  

James Elder afisa wa shirika la  Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto akiwa kituoni hapo alisema, ”idadi kubwa ya familia hizi walikuwa kwenye mahandaki jana usiku au siku mbili zilizopita. Hatimaye sasa wameweza kuelekea Poland.” 

Mwezi Machi, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Catherine Russell akihutubia Baraza la Usalama alisema makazi, shule, vituo vya yatima na hospitali vyote vimeshambuliwa. 

Mipakani maelfu ya watu walifurika kusaka kukimbia Ukraine, Shabia Mantoo kutoka shirika la Umoja wa  Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR akisema kwa kasi hiyo, bila shaka Ulaya inaelekea kukumbwa na janga kubwa la wakimbizi la karne hii.” 

Umoja wa Mataifa ukazindua ombi maalum la usaidizi kwa Ukraine mwezi huo wa Machi huku shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO likitangaza kuwa zaidi ya vituo 760 vya afya Ukraine vimeshambuliwa lakini Mkurugenzi wake Mkuu, Dkt. Tedros Ghebreyesus akasema licha ya mashambulizi, tunaanzisha njia ya kufikisha vifaa kwa ajili ya vituo vya afya nchini Ukraine. 

Huduma za afya ya uzazi nazo ziliimarishwa kama alivyosema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, Dkt, Natalia Kanem akiwa Moldova, moja ya nchi zilizopokea wakimbizi wengi kutoka Ukraine alisema “timu yangu inalinda wajawazito wasipate hatari yoyote wakijifungua hata katikati ya vita.” 

Katibu Mkuu António Guterres (katikati) akitembelea vitongoji vya makazi ya Irpin, katika Kyiv Oblast ya Ukraine.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu António Guterres (katikati) akitembelea vitongoji vya makazi ya Irpin, katika Kyiv Oblast ya Ukraine.

Baraza Kuu na Azimio la kulaani shambulio 

Hayo yakiendelea, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, Baraza Kuu likapitisha azimio la kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Nchi 141 zikiunga, 5 zikipinga na 35 hazikupiga kura kabisa. 

Mwezi Aprili Katibu Mkuu Antonio Guterres akatembelea Ukraine akajionea hali halisi ya uharibifu “kwenye vita, wanaoumia zaidi ni raia.”  

Kutoka hapo alikwenda Urusi akakutana na Rais Vladmir Putin ambaye kimsingi alikubali kuhamishwa kwa raia kutoka mtambo wa nyuklia Mariupol. Guterres alirejea tena Ukraine na kushuhudia usambazaji wa misaada ya kiutu. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO likageukia msaada kwa wakulima ambapo afisa wake Pierre Vauthier alisema,  ni muhimu sana sasa kusaidia wakulima. Kinachotia moyo ni kuona wananchi wa Ukraine wakijaribu kurejea katika maisha ya kawaida. Uwezo wao tu wa mnepo katika hali ya sasa.” 

Katibu Mkuu António Guterres akitazama nafaka zikipakiwa kwenye meli ya Kubrosliy mjini Odesa, Ukraine.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu António Guterres akitazama nafaka zikipakiwa kwenye meli ya Kubrosliy mjini Odesa, Ukraine.

Makubaliano ya usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi 

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ukasababisha uhaba wa chakula, nishati na mbolea duniani kutokana na meli za mizigo kushindwa kuingia na kutoka Ukraine moja ya nchi tegemeo duniani kwa bidhaa hizo!  

Mwezi Julai baada ya mazungumzo baina ya Urusi, Uturuki na  Ukraine, yakiratibiwa na Umoja wa Mataifa, mkataba wa usafirishaji nafaka kupitia baharí nyeusi ulitiwa saini, Guterres akiwa shuhuda. 

Na mwezi Septemba akihutubia Baraza Kuu la UN jijini New York, MArekani,  huku video ya meli ya shehena ya nafaka Brave Commander ikioneshwa, , Guterres alisema “meli hii ni ushahidi tosha wa kile tunachoweza kufanikisha tukishirikiana

Licha ya mafanikio katika usafirishaji wa nafaka nje ya Ukraine, changamoto ilisalia hofu ya mashambulizi dhidi ya mitambo ya nyuklia ukiwemo ule wa Zaporizhzhia na ndipo Guterres akasema, Bado nina hofu kuhusu hali katika mtambo huu wa Zaporizhzhia na viunga vyake, ikiwemo ripoti ya mashambulizi. 

Siku chache baadaye shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA, lilifika Ukraine ambapo Mkurugenzi wake mkuu Rafael Grossi alisema watahakikisha wanaweka ofisi ya kudumu ili kusimamia usalama na ulinzi. 

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi akitembelea na familia iliyokimbia makazi yao huko Lviv, Ukraine.
© Lviv State Oblast Administration
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi akitembelea na familia iliyokimbia makazi yao huko Lviv, Ukraine.

Ingawa hivyo mwaka mmoja hii leo, bado mashambulizi yanaendelea kama asemavyo Filippo Grandi kamishna mkuu wa UNHCR alipotembelea Ukraine akisema, “baada ya mwaka mmoja, nadhani tunaanza kuzoea hii hali. Hatupaswi kwa sababu inasikitisha kile ambacho uvamizi wa Syria unafanya kwa nchi hii.” 

Ndani ya mwaka mmoja wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, zaidi ya watu 8,000,000 wamekimbia nchi hiyo, zaidi ya 5,000,000 ni wakimbizi wa ndani ilhali theluthi moja ya wananchi wote hawako kwenye makazi yao. Watu milioni 17.6 wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu ambapo zaidi ya milioni 16 wameshafikiwa na msaada muhimu. 

Na sasa Katibu Mkuu Guterres ana kauli moja tu!  “vita hii lazima ikome!