Skip to main content

Njaa yashamiri Afrika, waathirika zaidi wakiwa ni Ukanda wa Afrika Mashariki

Wakulima nchini Rwanda na juhudi za kuimarisha ardhi.
© FAO/Petterik Wiggers
Wakulima nchini Rwanda na juhudi za kuimarisha ardhi.

Njaa yashamiri Afrika, waathirika zaidi wakiwa ni Ukanda wa Afrika Mashariki

Afya

Idadi ya watu wenye njaa barani Afrika inaendelea kuongezeka, ikichochewa na uwepo wa migogoro, mabadiliko ya tabianchi na kuzorota kwa uchumi sababu nyingine mbalimbali ikiwemo pia janga la COVID-19. Imesema ripoti iliyotolewa leo na viongozi wa mashirika matatu ya kikanda barani Afrika ambayo  yametoa wito wa kuchukua hatua zaidi juu ya mabadiliko ya mifumo ya kilimo.

Mashirika hayo matatu yaliyotoa ripoti hiyo ni pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO), Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) ambayo yametanabaisha kuwa hali ya uhakika wa chakula inazidi kuwa mbaya. 

Ripoti hiyo inayotoa ufahamu bora wa wigo wa njaa barani Afrika imetoa takwimu zinazoonesha kuwa mwaka 2020, Waafrika milioni 281.6 walikuwa na lishe duni, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 89.1 zaidi ya mwaka 2014. 

Kuna utofauti mkubwa katika viwango na mienendo ya njaa katika kanda ya Afrika, huku Afrika Mashariki ikiongozam kuwa na hali mbaya kwa kuwa na takriban asilimia 44 ya watu wenye lishe duni, asilimia 27 Afŕika Maghaŕibi, asilimia 20 Afŕika ya Kati, asilimia 6.2 Kaskazini mwa Afŕika, na asilimia 2.4 Kusini mwa Afŕika.

Hatua za muda mfupi za kukabiliana na changamoto ya njaa ni pamoja na nchi kutoa msaada wa kibinadamu pamoja na kuchukua hatua madhubuti za ulinzi wa kijamii. 

Na kwa hatua za muda mrefu, mashirika hayo yamesema nchi zitahitaji kuwekeza katika kilimo na sekta zinazohusiana, na vile vile katika huduma za maji, afya na elimu.

Mkurugenzi mkuu msaidizi wa FAO na Mwakilishi wa Kanda ya Afrika Abebe Haile-Gabriel amesema mikutano kadhaa iliyofanyika imetoa mapendekezo ya nini cha kufanya na kutoa wito kwa nchi za Afrika kutii wito wa mabadiliko ya mifumo ya chakula ili waweze kujinusuru “Nchi lazima zishiriki na kufanyia kazi matokeo ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula, Mkutano wa Lishe kwa Ukuaji na Mkutano wa 2021 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26)."
Naye William Lugemwa, ,mkurugenzi wa UNECA wa Idara ya maendeleo ya sekta binafsi na Fedha, pamoja na Josefa Sacko, Kamishna wa Muungano wa Afrika wa Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Bluu na mazingira endelevu, wameeleza kuwa "Dira ya pamoja, uongozi dhabiti wa kisiasa na ushirikiano mzuri wa sekta mbalimbali, unaojumuisha sekta binafsi, ni muhimu ili kukubaliana juu ya biashara na kutambua na kutekeleza masuluhisho endelevu ambayo yanabadilisha mifumo ya kilimo." 

Njaa katika bara la Afrika imekuwa mwiba tangu mwaka 2013, na kuzorota zaidi kati ya 2019 na 2020 huku hali ikitarajiwa kuwa mbaya zaidi mwaka huu, huku kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kupunguza njaa.