Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika lazima iimarishe haraka mifumo ya chakula ili kujikwamua vyema na COVID-19: IFAD/ADB

Mama Veronique akivuna mazao aliyopanda.
UNICEF/UNI212593/Tremeau
Mama Veronique akivuna mazao aliyopanda.

Afrika lazima iimarishe haraka mifumo ya chakula ili kujikwamua vyema na COVID-19: IFAD/ADB

Ukuaji wa Kiuchumi

Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD na Benki ya Maendeleo Afrika ADB, kwa kushirikiana na jukwaa kwa ajili ya utafiti wa kilimo Afrika FARA, wanaendesha mazungunmzo ya ngazi ya juu ya siku mbili yenye lengo la kulichagiza bara la Afrika kuhakikisha linajikwamua vyema na janga la corona au COVID-19 kwa kuwekeza na kuimarisha mifumo yake ya chakula kuepuka baa la njaa.

Majadiliano hayo kwa njia ya mtandao yalioyanza leo 29 Aprili na kutarajiwa kukamilika kesho Aprili 30 yamebeba mada ya “Kuilisha Afrika:uongozi katika kusongesha mafanikio ya ubunifu” , yamewaleta pamoja viongozi wakuu wa nchi na serikali, maafisa wa ngazi ya juu wa serikali, wakuu wa benki za kimataifa za maendeleo, wadau wa maendeleo, mashirika ya kikanda, taasisi za utafiti, viongozi wa sekta za biashara, sekta binafsi, mashirika ya uwekezaji, wanazuoni, mashirika ya asasi za kiraia na wataalam kutoka barani Afrika na kwingineko. 

IFAD na ADB wanasema licha ya mafanikio mazuri na yanayoendelea katika maendeleo ya uchumi katika nchi nyingi za Afrika, bado tatizo la njaa linaongezeka na kuathiri watu milioni 246 barani humo. 

Wameongeza kuwa janga la COVID-19 limedhihirisha nyufa zilizoko katika mifumo ya chakula  ya barani hilo ambayo tayari iko katika shinikizo kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, vita na wadudu waharibifu kama nzige. 

Kwa mantiki hiyo  wamesisitiza kwamba “Kinachohitajika ni kuongeza uwekezaji na kupanua wigo wa ushirika haraka ili kuchagiza mabadiliko katika kilimo Afrika kupitia teknolojia na ubunifu.” 

Na mabadiliko hayo IFAD na ADB wanasema ni pamoja na kuimarisha mifumo ya chakula kama sehemu ya kujikwamua vyema na janga la COVID-19 lakini pia kujenga mnepo wa kukabiliana na tatizo la njaa. 

Majadiliano hayo yanalenga kupata ahadi za kisiasa kutoka kwa viongozi ili kuhakikisha mafanikio barani kote, kubadilishana uzoefu, kuonyesha yale yanayozaa matunda katika utafiti na maendeleo ya kilimo, nini kinachohitajika kufanyika ili kuwa na uwekezaji endelevu na kufikia mtazamo wa pamoja kkuanzia masuala ya uwekezaji hadi teknolojia ya uzalishaji na ubunifu utakaobadili mifumo ya chakula ya Afrika. 

Na tamko litakalotolewa kesho katika mwisho wa majadiliano hayo litatumiwa kuchangia kwenye mkutano wa awali wa mifumo ya chakula unaotarajiwa kufanyika Julai mjini Roma Italia na ule mkubwa wa  Umoja wa Mataifa wa mifumo ya chakula utakaokuwa baadaye mwaka huu.