Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataja mambo manne ya kuzingatia kuleta ujumuishi, amani na usawa duniani

Baraza la Usalama likiwa limekutana kujadili masuala ya wanawake na amani na usalama ( Maktaba)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Baraza la Usalama likiwa limekutana kujadili masuala ya wanawake na amani na usalama ( Maktaba)

Guterres ataja mambo manne ya kuzingatia kuleta ujumuishi, amani na usawa duniani

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa , leo limekutana katika mjadala wa wazi kwenye makao Makuu mjini New York Marekani kuangazia ukarabati wa amani ya kimataifa na usalama , hasa katika upande wa kubaguliwa, kutokuwepo na usawa na migogoro. 

Akizungumza katika mjadala huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kwa watu masikini zaidi na walio hatarini zaidi, janga la coronavirus">COVID-19 limeongeza huzuni na ukosefu wa usawa. 
“Takriban watu milioni 120 zaidi wamesukumwa katika umaskini. Ukosefu wa chakula na njaa vinanyemelea mamilioni ya watu kote ulimwenguni. Tunakabiliwa na mdororo mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani tangu vita vya pili vya dunia.” 

Ameongeza kuwa mabilioni ya watu wanakosa ulinzi wa hifadhi ya jamii wanaohitaji ili kuhimili hali ya maisha ikiwemo huduma za afya na ulinzi wa ajira. 

Katibu mkuu akaenda mbali zaidi  na kusema “Watu katika nchi tajiri zaidi wanapata dozi ya tatu ya chanjo ya COVID-19, wakati ni asilimia tano tu ya Waafrika wamechanjwa kikamilifu. Hata kabla ya janga hili, mabilionea wa ulimwengu walikuwa na utajiri zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu  wote duniani na pengo hilo limeongezeka sana.” 

Amesisitiza kuwa "Utajiri hauambukizi. Kutengwa na ukosefu wa usawa wa kila aina  kuanzia kiuchumi, kijamii na kitamaduni  huja na athari mbaya kwa usalama. Kwa hakika kuongezeka kwa pengo la usawa ni chachu kubwa ya kuongezeka kwa migogoro” 

Kukosa huduma za msingi hakuvumiliki 

Bwana Guterres amesema hususan katika maeneo ambako huduma za msingi kama afya, elimu, usalama na haki vinakosekana machafuko na ukosefu wa usalama haviko mbali. 

Mbali ya hayo ameongeza kuwa katika maeneo ambako kihistoria hakuna haki, pengo la usawa limetawala na ukandamizaji wa kimfumo wamevifunga vizavi na watu wa maeneo hayo katika mzunguko wa kutopata mafanikio na umasikini. 

Amelikumbusha Baraza kwamba “Leo hii dunia inakabiliwa na idadi kubwa ya machafuko na vita tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia mwaka 1945, inadumu kwa muda mrefu na ina athari kubwa.” 

Hali ya hatari ya ukwepaji wa sheria inaendelea kutanda na inaonekana katika unyakuzi wa hivi karibuni wa mamlaka kwa nguvu, ikiwa ni pamoja na mapinduzi ya kijeshi. 

Guterres pia amesema “Haki za binadamu na utawala wa sheria vinashambuliwa kuanzia Afghanistan, ambapo wasichana wananyimwa haki ya elimu  na wanawake wananyimwa nafasi zao katika jamii, nako Myanmar, ambapo watu wachache wanalengwa, wanateswa kikatili na kulazimika kutoroka.”

Ameongeza kuwa nchini Ethiopia, tunashuhudia mzozo wa kibinadamu unaosababishwa na binadamu ukitamalaki mbele ya macho yetu. 
Amesema haya na majanga mengine yamechochewa na COVID-19 na dharura ya za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba “Amani haijawahi kuwa ya dharura zaidi kama ilivyo sasa kuliko wakati mwingine wowote. Bila kujumuishwa, fumbo la amani bado halijakamilika, na mapengo mengi yanapaswa kuzibwa.” 

Mambo manne ya kuzingatia katika ujumuishwaji 

Katibu Mkuu ameainisha masuala manne katika njia ya ujumuishwaji , ili kuweza kuziba mapengo  ambayo yanajikita na watu, uzuiaji, jinsia na taasisi. 

Mosi - tunahitaji kuwekeza katika maendeleo ya watu wote, kwa usawa. 
Pili  - tunahitaji kuimarisha ajenda yetu ya kuzuia katika nyanja mbalimbali ili kushughulikia aina tofauti za ubaguzi na ukosefu wa usawa. 
Tatu - ni lazima kutambua na kutoa kipaumbele katika nafasi muhimu ya wanawake katika ujenzi wa amani. 
Nne - ni lazima tujenge uaminifu kupitia taasisi za kitaifa zinazojumuisha na kuwakilisha watu wote, zinazozingatia haki za binadamu na utawala wa sheria.