Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shida na changamoto nyingi zinazowakumba wanawake ni kutokana na mfumo dume na uchu wa madaraka: Guterres

Mwakilishi mwanamke akichagiza wanawake wengine kupaza sauti zao Rajasthan, India.
UN Women/Ashutosh Negi
Mwakilishi mwanamke akichagiza wanawake wengine kupaza sauti zao Rajasthan, India.

Shida na changamoto nyingi zinazowakumba wanawake ni kutokana na mfumo dume na uchu wa madaraka: Guterres

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema pamoja na kuwepo kwa maazimio na sheria nyingi za kuhimiza usawa kwenye jamii, wanawake na wasichana kila kona ya dunia wanaendelea kuteseka, kunyanyasika na kuonewa na yote haya ni kutokana na kuwepo kwa mizizi ya mfumo dume na uchu wa madaraka.

Usawa kwa wanawake ni suala la madaraka .... ni Katibu Mkuu Antonio Guterres akizungumza katika mjadala kuhusu kutimiza ahadi: Jukumu la mashirika ya kikanda katika kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama panapoibuka mizozo ya kisiasa na utwaaji wa madaraka kimabavu. uliofanyika hii leo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika makao Makuu jijini New York, Marekani. Amesema tayari inafahamika kuwa usawa wa kijinsia unatoa njia bora kwa amani endelevu na kuzuia migogoro, na bado dunia inazidi kurudi nyuma kutokana na ukosefu wa usawa wa kijinsia, umasikini, mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa. “Katika baadhi ya nchi, itikadi kali, na uongozi wa mabavu wa kijeshi umechukua mamlaka kinguvu na kufuta ahadi zote zilizowekwaa awali za usawa wa kijinsia na kuwanyima wanawake hata haki za kuendelea na maisha yao ya kilasiku.“ Amezitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Afghanistan, Mali, Myanmar, Sudan pamoja na Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. “Katika migogoro yote hii tunaona wanaume wakiwa madarakani na wanawake wametengwa, haki zao na uhuru wao unalengwa kwa makusudi.” Guterrs amesema ulimwenguni kote, mabadiliko ya hivi karibuni ya kuachana na siasa-jumuishi yanaonesha kwa mara nyingine tena kwamba “chuki dhidi ya wanawake na ubabe vinazidi kuimarika na hii ni kinyume na jamii zilizo imara na zenye ustawi.” Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kufurahishwa na ushirikiano unaooneshwa na Muungano wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Umoja wa Nchi za Kiarabu na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya katika ajenda ya wanawake, amani na usalama kwa vitendo kupitia kazi wanazozifanya mashinani na sio taarifa na maazimio pekee.