Ubinafsi wa chanjo za COVID-19 unaofanywa na matajiri si sawa:Museveni

24 Septemba 2021

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ameuambia mjadala mkuu wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa au UNGA76 kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kuhakikisha changamoto zilizopo ikiwemo janga la corona au COVID-19 kwa kuacha suala la ubinafsi hasa katika upatikanaji wa chanjo kwani makosa makubwa sana. 

Katika hotuba yake kwenye mjadala huo aliyoitoa kwa njia mtandao, Rais Museveni akatoa wito “Kwa hivyo, tunatoa wito kwa hatua zaidi kuhakikisha kuwa katikati ya dunia kujikwamua na janga hili la COVID-19 , kuwe na usawa na ufikiaji nafuu kwa wote wa chanjo salama, bora, zinazofaa, zinayoweza kupatikana, za bei rahisi, tiba na uchunguzi. Tunapongeza juhudi za Katibu Mkuu ( wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres) kwa kuendelea kwake kutetea na kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo.” 
  
Kwa upande mwingine, amessisitiza “tunaona kwamba hatua za wengine kuhodhi chanjo kwa gharama ya maisha ya watu wa nchi masikini, ambazo pia hujulikana kama ubinafsi wa chanjo, sio sawa, lakini somo zuri kwa nchi zinazoendelea ambazo hazitaki kuwa wabunifu. Ni somo zuri kwa sababu huwaamsha wale ambao wamelala, wakingojea kuokolewa na wengine.” 

Ameongeza kuwa Uganda inaendelea kutafuta tiba na chanjo, ambazo zitapatikana katika miaka michache. “Tunatengeneza chanjo kwa ufadhili wetu wenyewe na msaada ambao tunahitaji ni kwa malighafi ya chanjo. Kwa hivyo, tunaalika washirika wanaovutiwa kutusaidia na malighafi.” 

Wagonjwa wakisubiri chanjo ya COVID-19 katika kituo cha afya wilayani Kabale, Uganda
© UNICEF/Catherine Ntabadde
Wagonjwa wakisubiri chanjo ya COVID-19 katika kituo cha afya wilayani Kabale, Uganda

Malengo ya maendeleo endelevu SDGs 

Kuhusu malengo ya maendeleo endelevu au SDGS, Rais Museveni amesema Uganda inasisitiza tena kujitolea kwake kutekeleza ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu kwa ukamilifu na kufikia malengo yote 17 tunapoanza miaka kumi ya utekelezaji na utimizaji wa maendeleo endelevu.  

Ameongeza kuwa “Sasa tumegundua zaidi ya wakati mwingine wowote, hitaji la haraka la kuharakisha maendeleo yetu kuelekea utekelezaji wa Ajenda ya 2030 kama nguzo katika hatua zetu za kitaifa za kupambana na athari nyingi za janga la COVID-19 tunapojijenga vyema na kujitahidi kufikia lengo kuu la ajenda ya 2030 ya kutokomeza umasikini katika aina na vipimo vyake vyote.” 

COVID-19 inaimarisha vizuizi vilivyotangulia kufikia Malengo, usawa wa muundo, mapungufu, changamoto za kimfumo na hatari. Tunaamini kabisa kuwa kufanikiwa kwa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Kitaifa (NDP III) chini ya kaulimbiu "Viwanda endelevu vya ukuaji unaojumuisha, ajira na uzalishaji mali" ni muhimu katika kufanikisha malengo yote 17 ya SDGs. 

Amesema Janga la COVID-19 limevuruga maendeleo ya Uganda katika baadhi ya sekta lakini pia limetoa msukumo na fursa kwa harakati za viwanda nchini humo. Athari ambazo janga hili limesababisha kwenye ajira, hadi sasa katika sekta mbalimbali zinaweza kuathiri sana juhudi za kupunguza umaskini, kusababisha mazingira magumu na ukosefu wa usawa.  

Hata hivyo amesema zimeamsha mjadala juu ya jinsi Uganda inavyojenga mifumo yake ili kutoa ushujaa unaohitajika kuhimili mshtuko kama huo. 

Nchini Uganda, mpango wa kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa hali ya hewa, maji na hali ya hewa unaendelea.
UNDP/Andrea Egan
Nchini Uganda, mpango wa kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa hali ya hewa, maji na hali ya hewa unaendelea.

Mabadiliko ya tabianchi 

Rais Museveni amesema kuweka njia yetu kuelekea utimilifu kamili wa ajenda ya 2030 na Mkataba wa Paris “inahitaji tushughulikie haraka mabadiliko ya tabianchi  na upotezaji mkubwa wa maisha na mali kwa sababu ya majanga yanayohnusiana na mabadiliko ya tabianchi duniani. Sisi sote tunahusika na majanga haya ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa hivyo, tunasisitiza hitaji la kuimarisha mwitikio wa kimataifa kwa tishio la mabadiliko ya tabianchi katika muktadha wa maendeleo endelevu na juhudi za kutokomeza umasikini kupitia hatua za ujasiri za pande zote.”  

Uganda inaendelea kupata ukame wa muda mrefu, kuyeyuka kwa barafu kwenye mlima wake mrefu, Mlima Ruwenzori, mafuriko, mvua ya kawaida na maporomoko ya ardhi. 

Hivi karibuni, Uganda ilipata athari za ukame na mvua ya muda mrefu, na kuathiri sana maisha na uwezo wa watu kuishi.  

Rais huyo wa Uganda ameongeza kuwa tunashiriki ziwa Victoria, ziwa la pili kwa ukubwa la maji safi, na nchi za Jirani za Kenya na Tanzania. Kiwango cha maji ya ziwa hilo nchini Uganda hupimwa mahali katika jiji la Jinja na kiwango cha chini kabisa cha maji kuwahi kurekodiwa ilikuwa mnamo 1923, wakati ilikuwa mita 10.28. 

Kabla ya hapo, kiwango cha juu kabisa kilichorekodiwa kilikuwa mnamo Januari 1 mwaka 1918; rekodi ilionyesha mita 11.89 na rekodi ya kiwango cha juu iliyofuata ilikuwa Mei 16, 1964, wakati kiwango cha maji kilifikia mita 13.41. 

Lakini, amesema tangu mwaka jana, kiwango cha maji katika ziwa kimekuwa kikipanda. Mei 19, 2020, kiwango cha maji kilifikia rekodi  mpya ya mita 13.49. Tangu wakati huo, kiwango cha maji kimebaki juu ya mita 13. Kwa hivyo, tumewataka watu ambao wanakaa karibu sana na ziwa wahamie mbali na ziwa na eneo la pwani. Kukaa mita 200 kutoka Ziwa ni jambo la busara, sahihi na muhimu kufanya. 

Amesisitiza kuwa ingawa Uganda si mchangiaji mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi lakini ni miongoni mwa waathirika wa athari zake. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter