Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nishati jadidifu ni chachu ya maendeleo na mustakbali wa amani:UNEP

Mtaalam akitembelea paneli za sola zilizowekwa katika moja ya paa za ghala mjini Lusaka zambia
UNDP/Karin Schermbrucker
Mtaalam akitembelea paneli za sola zilizowekwa katika moja ya paa za ghala mjini Lusaka zambia

Nishati jadidifu ni chachu ya maendeleo na mustakbali wa amani:UNEP

Tabianchi na mazingira

Nishati mbadala au jadidifu ni "muhimu kwa kujenga mustakbali endelevu, ustawi na amani", amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizindua harakati za kuongeza kasi kwa ajili ya nishati safi na hatua kwa ajili ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Antonio Guterres ameyasema hay oleo jumatano na kuongeza kwamba "Changamoto yetu iko bayana, ili kufikia kiwango cha kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050, dunia lazima ipunguze uzalishaji wa hewa ukaa kwa angalau asilimia 45 chini ya viwango vya mwaka 2010 katika muongo mmoja ujao".

Katibu Mkuu alikuwa akihutubia kwa njia ya mtandao zaidi ya mawaziri 20 "Mabingwa wa Ulimwenguni" katika mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu nishati likiwa ni jukwaa la kimataifa ambapo serikali, wafanyabiashara na wengine wanaweza kukusanyika ili kupendekeza matumizi ya nishati endelevu.

Guterres amesisitiza kuwa dunia hivi sasa imetoka nje ya msitari na inahitajika kutumia kipindi cha kujikwamua na janga la COVID-19 kujenga uchumi endelevu, unaongozwa nanishati jadidifu.

"Ikiwa tunataka mabadiliko haya ya nishati kuwa ya haki, na kufanikiwa katika kuunda ajira mpya, mazingira safi na yenye afya na mustakabali mzuri wenye mnepo, nchi zinazoendelea zinahitaji msaada mkubwa".

Kuelekea mkutano wa nishati unaotarajiwa mwezi Septemba, Bwana Guterres aliona mazungumzo haya kama fursa ya "kuharakisha upelekaji wa nishati jadidifu ulimwenguni na kuhakikisha kwamba nchi zinazoendelea zinaipata".

India na Honduras, kupitia ushirikiano wa nchi za kusini, SSC, zimekuwa zikifanya kazi pamoja kuimarisha matumizi ya vyanzo vyao vya nishati jadidifu.
UNDP Honduras
India na Honduras, kupitia ushirikiano wa nchi za kusini, SSC, zimekuwa zikifanya kazi pamoja kuimarisha matumizi ya vyanzo vyao vya nishati jadidifu.

Kufanya kazi pamoja

Vikundi vitano vya masuala ya kiufundi vitatayarisha mwongozo wa kimataifa wa kufanikisha lengo la saba la maendeleo endelevu (SDG 7) la nishati safi na nafuu kwa wote ifikapo mwaka 2030 na kuutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050. 

Kwa kuwa matumizi ya nishati yanachangia robo tatu ya uzalishaji wote wa gesi chafuzi ya viwandani, pia yatachangia kushughulikia mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi. 

Na katika miezi ijayo, mawaziri wa mabingwa wa dunia watasisitiza ahadi za nguvu za hiari kuelekea kufanikisha lengo la SDG 7, ambalo litalingana na mipango ya nchi kuziweka katika kuongeza hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, au michango ya kitaifa (NDCs), na malengo ya mabadiliko ya tabianchi ya muda mrefu chini ya mkataba wa Paris 2015. 

Katika mwaka huu wa mpito, mwenyekiti mwenza wa majadiliano ya ngazi ya juu  na mwakilishi maalum kwa ajili ya nishati endelevu kwa wote amesisitiza haja ya hatua za ujasiri ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyite aliyeachwa nyuma.

"Kuanzia kutoa nishati kwa vituom vya afya hadi kuunda ajira mpya, nishati ni kiini cha mustakabali mzuri kwa wote", amesema Damilola Ogunbiyi, ambaye pia ni bingwa wa ngazi ya juu.

 "Maendeleo ya haraka ya lengo la SDG 7 yatasaidia hatua za mabadiliko ya tabianchi, kuturuhusu kujikwamua vyema kutoka kwa janga la COVID-19 na kufikia malengo yetu ya maendeleo ya ulimwengu."

Zaidi ya athari za kimazingira kuendelea kutumia nishati ngumu ya kupikia majumbani inasababisha vifo vya mapema takriban milioni 1.6 kila mwaka huku wengi wakiwa ni wanawake na watoto , kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.