Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afcon: Shamrashamra zagubikwa na ukimbizi na njaa mashariki mwa DRC

Wakazi wa kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwa kwenye tamasha la mpira wa soka lililoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, na kufanikishwa na WFP.
© WFP/Michael Castofas
Wakazi wa kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwa kwenye tamasha la mpira wa soka lililoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, na kufanikishwa na WFP.

Afcon: Shamrashamra zagubikwa na ukimbizi na njaa mashariki mwa DRC

Msaada wa Kibinadamu

Huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC shamrashamra za mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika, Afcon yanayoendelea huku Côte d'Ivoire zinagubikwa na ukimbizi na ongezeko la matukio ya ukatili wa kingono huku shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP likichukua maamuzi magumu kutokana na ukata unaokabili operesheni zake. 


 

Natasha Nadazdin ambaye ni Naibu Mwakilishi Mkazi wa WFP nchini DRC akiwa Kinshasa anasema ingawa macho na masikio yanaelekezwa kwenye mashindano hayo adhimu kwa Afrika, DRC ikiwa ni moja ya washiriki, ni vema kutafakari kile kinachokumba watoto wa DRC na dunia nzima kwa ujumla, ili iwapo wangepatiwa lishe, elimu na mafundo wanayohitaji ili kuweka mazingira sawa ndani na nje ya uwanja wa soka.  

Kulikoni suala hili zito haligongi vichwa vya vyombo vya habari kimataifa? 

Kupitia wavuti wa WFP, Bi. Nadazdin anasema DRC pamoja na Afghanistan, Yemen na Syria ni miongoni mwa mataifa yanayokumbwa na dharura kubwa zaidi kutokana na miongo kadhaa ya mapigano na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kupunguza fursa ya watu kupata mlo na hivyo kusababisha njaa kufikia viwango vya juu zaidi. 

Afisa huyo wa WFP anasema, hali ni mbaya DRC, watu wanakumbwa na changamoto nyingi na cha kusikitisha ajenda ya changamoto za DRC  si ajenda kwenye vyombo vya habari vya kimataifa. Mamilioni  ya watu wako kwenye hatari na makumi ya makundi yaliyojihami yanagombania utajiri wa taifa hilo. Barabara na madaraja mara nyingi huharibiwa au huwekewa vizuizi na hivyo kukwamisha vyakula kuharibika au safari kuwa ndefu kufikisha chakula

Zaidi ya watu milioni 6 ni wakimbizi wa ndani na hawana tena mbinu za kujipatia kipato, miongoni mwao ni 720,000 waliokimbia makwao tangu mwezi Oktoba mwaka jana. Taarifa za wanawake na wasichana kubakwa zinaongezeka huku ukosefu wa utawala wa sheria ukitumbukiza makumi ya maelfu kwenye ukatili wa kijinsia. 

“Kadri WFP inavyohaha kukabiliana na uhaba wa ufadhili duniani na ongezeko la mahitaji  ya kibinadamu, simulizi za kutisha – ukatili wa kingono – zinazoibuka huko mashariki mwa DRC zinahitaji swali jepesi: ni kwa vipi janga lenye kiwango kama hicho halipatiwi kipaumbele cha kutosha?” anahoji Afisa huyo wa WFP. 

Ufe njaa au ukumbwe na ukatili wa kingono upate mlo 

Wanawake wanaoishi kwenye kambi za wakimbizi wana chaguo lisilo la kawaida la kuacha familia zao zife njaa au wakumbwe na ukatili wa kingono pindi wanapokwenda kusaka chakula au kuni, na penginepo wakubali mikakati isiyo salama ya kutumikishwa kwenye ukahaba ili mlo uende kinywani. 

Sababu lukuki ndio chanzo cha ongezeko la matukio ya ukatili wa kingono: kuanzia ukosefu wa usawa wa kijinsia, utamaduni wa kukwepa sheria, mfumo dhaifu wa haki, kufurushwa makwao na mazingira yasiyo salama ya kuishi hadi njaa na umaskini, ukosefu wa fursa za kufikia chakula na ufadhili usiotosheleza kwa ajili ya operesheni za misaada ya kiutu. 

Mbinu zenye utaratibu na zinazofahamika zinaweza kupunguza mikakati hii ya kuweza kuishi DRC. Bi. Nadazdin  anasema “sisi katika WFP tuko makini kuangazia uhusiano kati ya ukosefu wa uhakika wa kupata chakula na ongezeko la hatari wanazokumbwa nazo wanawake Mashariki ya DRC pindi wanapokosa ulinzi. Ingawa kuwapatia msaada wa chakula na mahitaji mengine kama vile malazi, maji na huduma za kujisafi ni muhimu, uchechemuzi wa pamoja, mipango na majawabu jumuishi vinahitajika huku wadau wengi zaidi na washirika wakijumuishwa. 

Nafasi ya Mashariki ya DRC kuleta utulivu na maendeleo 

WFP inasema ingawa ni muhimu kutambua mazingira tofauti tofauti na magumu ya kila eneo, kusaka suluhu kwenye majimbo yenye mapigano ni muhimu, mathalani Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ili hatimaye hali hiyo ichangie kwenye utulivu na maendeleo ya DRC.  

Na hilo inasema itahitaji amani na kurejea kwa usalama makwao wakimbizi wa ndani. 

“Wakirejea kwenye ardhi yao, kazi yao inaweza kuvutia uwekezaji kwenye miundombinu ya vijijini na kujenga shughuli za kuwapatia mnepo. Hii pia itahitaji kuwajumuisha kwenye jamii wapiganaji ili hatimaye DRC iweze sio tu kujilisha chakula lakini vile vile kuuza nje ya nchi  mazao.” 

Sasa WFP inahitaji nini kwa kipindi cha miezi sita? 

WFP  inahitaji jumla ya dola milioni 567.8 kwa ajili ya operesheni zake nchini DRC na kwa kuwa kuna pengo sasa, “tunafanya kile tunachoita kipaumbele cha kupitiliza: Kupatia wahusika mgao kamilifu wa miezi 6 kwa idadi kidogo ya watu badala ya kusambaza kiwango kidogo cha chakula ambacho hakitoshelezi. Ni uamuzi wenye uchungu, na ndio maana tunahitaji haraka fedha.”