Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twahitaji dola milioni 567 kufanikisha operesheni Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini- WFP

Akina mama waliokimbia makazi na wanawake wajawazito wakitafuta usaidizi wa WFP katika kambi ya wakimbizi huko Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC.
© WFP/Michael Castofas
Akina mama waliokimbia makazi na wanawake wajawazito wakitafuta usaidizi wa WFP katika kambi ya wakimbizi huko Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC.

Twahitaji dola milioni 567 kufanikisha operesheni Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, linasema linahitaji dola milioni 567 kukidhi mahitaij ya wananchi kwenye majimbo matatu kwa miezi sita ijayo - Agosti 2023 hadi Januari 2024. 

Taarifa ya WFP kutoka Kinshasa, DRC inasema ombi hilo ni kwa ajli ya watu milioni 3.6 walioko majimbo hayo matatu ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ambao wana uhitaji zaidi. 

“Katika majimbo hayo yaliyoko mashariki mwa nchi, jumla ya watu milioni 6.7 wanakabiliwa na ukosefu wa uhakika wa kupata chakula,” imesema taarifa hiyo, ikitaja ukosefu wa usalama na mapigano kuwa sababu ya uhaba huo. 

Wahitaji hao sio tu wale walioathiriwa na mapigano ambao ni wakimbizi wa ndani bali pia na wakazi wengine wa maeneo hayo. 

Licha ya operesheni ya usaidizi iliyotangazwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwenye eneo hilo bado mahitaij ni makubwa kuliko rasilimali zilizoko. 

Mathalani WFP inajitahidi kusambaza msaada wa vyakula na fedha taslimu kwa wahitaij lakini bado hazitoshelezi kwani ufadhili unasuasua.