Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunalaani vikali shambulio dhidi ya MONUSCO Kivu Kaskazini:UN 

Helikopta ikipaa kutoka katika kambi ya MONUSCO mjini Beni, Kivu Kaskazini. (Maktaba)
MONUSCO/Abel Kavanagh
Helikopta ikipaa kutoka katika kambi ya MONUSCO mjini Beni, Kivu Kaskazini. (Maktaba)

Tunalaani vikali shambulio dhidi ya MONUSCO Kivu Kaskazini:UN 

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio lililofanyika jana Jumatatu dhidi ya eneo la muda la mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC katika mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo na msemaji wake, shambulio hilo linashukiwa kufanywa na vwapiganaji wa Allied Democratic Forces ADF, na limesababisha kifo cha mlinda amani mmoja kutoka Malawi. 

Katibu Mkuu anatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu mlinda amani huyo, na pia kwa Serikali na watu wa Malawi. 

Pia “Amekumbusha kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuunda uhalifu wa kivita na anatoa wito kwa mamlaka ya DRC kuchunguza tukio hili na kuwafikisha haraka wale waliohusika kwenye mkono kwa sheria” 

Bwana Guterres amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa, kupitia mwakilishi wake maalumJamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wataendelea kuunga mkono Serikali ya DRC na watu wake katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu Mashariki mwa nchi hiyo. 

Nalo Baraza la Udsalama la Umoja wa Mataifa katika taarifa yake ya kulaani shambulio hilo limesema “Wajumbe wa Baraza  la Usalama wamesisitiza umuhimu wa MONUSCO kuwa na uwezo unaohitajika kutimiza majukumu yao na kuchagiza usalama na ulinzi wa walindaamani wa Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia maazimio ya Baraza hilo.” 

Pia wajumbe wamerejea kusisitiza msaada wao kwa mpango wa MONUSCO na vikosi vyake na kutoa shukran za dhati kwa vikosi hivyo vya MONUSCO nan chi zinazochangia vikosi wakiwemo polisi.