Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani mauaji ya raia 55 yaliyofanywa na ADF mashariki mwa DRC 

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO wakifanya doria katia eneo la Ituri ili kuzuia vitendo vya ADF.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO wakifanya doria katia eneo la Ituri ili kuzuia vitendo vya ADF.

UN yalaani mauaji ya raia 55 yaliyofanywa na ADF mashariki mwa DRC 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio ya siku ya Jumatatu yaliyofanywa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) dhidi ya wakimbizi wa ndani huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kusababisha vifo vya raia 55 na wengine wengi wamejeruhiwa.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumanne usiku jijini New York, Marekani imesema waasi hao wa ADF walishambulia kambi za wakimbizi wa ndani zilizoko karibu na mji wa Boga jimboni Ituri na  mji wa Tchabi jimboni Kivu Kaskazini na kuua raia hao 55. 

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliouawa kwenye mashambulizi hayo huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi. 

Ametoa wito kwa mamlaka za DRC kuchunguza haraka matukio hayo na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, ulipelekwa kwenye miji hiyo ambako walinda amani wanapatia huduma majeruhi sambamba na kusafirisha wale wanaohitaji huduma zaidi za matibabu. 

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa kupitia mwakilishi wake maalum nchini DRC, utaendelea kusaidia serikali ya DRC na wananchi wake katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa taifa hilo.