Jukwaa la kudumu la watu wa asili la UN limetambulisha uwepo wetu Watwa wa Burundi - Vital Bambanze

Mkurugenzi wa UNIPROBA, shirika lililoundwa na Batwa kwa ajili ya Batwa nchini Burundi.
UN/Assumpta Massoi
Mkurugenzi wa UNIPROBA, shirika lililoundwa na Batwa kwa ajili ya Batwa nchini Burundi.

Jukwaa la kudumu la watu wa asili la UN limetambulisha uwepo wetu Watwa wa Burundi - Vital Bambanze

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kikao cha 20 cha Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la watu wa asili kinaanza rasmi leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na mtandaoni na litaendelea hadi tarehe 30 Aprili.

Jukwaa hilo linalofanyika kila mwaka na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza kuu, nchi wanachama na wadau mbalimbali  wa masuala ya asili, mwaka huu linajikita katika mada ya amani, haki na taasisi imara: jukumu la watu wa asili katika utekelezaji wa lengo namba 16 la maendeleo endelevu au SDGs.   

Kama ilivyo ada ya kila mwaka pamoja na kujikita na mada maalum washiriki wanatathimini hatua zilizopigwa katika masuala kama haki za binadamu, mabadiliko ya tabianchi, uwakilishi na utawala kwa ajili ya watu wa asili kutokana na ripoti mbalimbali zilizoandaliwa. 

Miongoni mwa waliofika mjini New York Marekani kuhudhuria kikao hiki cha watu wa asili ni Vital Bambanze, Mwakilishi wa Watwa ambao ni jamii ya asili nchini Burundi. 

Bwana Bambanze akizungumza na Anold Kayanda wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema haki za Watwa zilikuwa zimewekwa mbali, watoto hawasomi, hawateuliwi kama viongozi, “hapo sasa unaona kwamba haki zetu zilikuwa hazijawekwa mbele. Sasa tukija katika mikutano kama hii, ni kukutana na watu mbalimbali na kuwajulisha kuwa haki zetu zinapaswa kutimizwa. Tunaowauliza kwanza ni viongozi wa nchi, lakini tukija hapa, tunakuja kukutana na watu wengine wa asili kutoka nchi nyingine na hapo tunabadilishana uzoefu na pia unakuwa wakati wa kuongea na watu ambao wanaweza kutoa misaada mbalimbali ya kusaidia watu wa asili ili haki zao zitimizwe kwa ajili ya maendeleo kwa ujumla.” 

Mkurugenzi wa UNIPROBA, shirika lililoundwa na Batwa kwa ajili ya Batwa nchini Burundi.
UN/Assumpta Massoi
Mkurugenzi wa UNIPROBA, shirika lililoundwa na Batwa kwa ajili ya Batwa nchini Burundi.

 

Na kuhusu ni ujumbe gani amekuja nao katika mkutano wa mwaka huu akiwawakilisha tena watu wa jamii yake ya Watwa, Bwana Bambanze anasema, “ujumbe ni ule ule kuonesha kuwa watu wa jamii asili wana haki asilimia 100 kama wananchi wengine. Mimi kama mtu kutoka Afrika, pia ujumbe wangu ni kuonesha kuwa kuna haki tunazozitaka. Haki ya kwanza ni ardhi kwa sababu watu wengi kutoka jamii ya watu wa asili hawana ardhi, hawapati elimu vizuri, na hawapati uongozi kama watu wengine, huo ndio ujumbe wangu wa kwanza.” 

Bwana Bambanze anataja ujumbe mwingine aliokuja nao kuondoa mtazamo ambao Watwa wanatazamwa kama watu ambao hawana mchango wowote kwa maendeleo, “sisi kama watu wa asili tunaishi kwa kuilinda misitu na mazingira na hali hiyo inapunguza mabadiliko ya tabianchi na kwa hivyo kama tunachangia hivyo basi na huu mchango wetu uonekane kwa kuleta faida kwa familia za watu wa asili. Ujumbe mwingine ni kuwaambia wanaotoa misaada watizame hiyo misaada yao kuwa inawafikia watu ambako umaskini unaonekana.” 

Tweet URL

Kama ilivyo mada ya mkutano wa mwaka huu ambayo ni inalenga mchango wa watu wa asili katika kutimiza lengo namba 16 la Malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu, Mwakilishi huyu wa jamii ya Watwa wa Burundi anaongeza kusema kuwa sasa wanataka kuonesha kwamba kama hakuna amani, kama hakuna haki, maendeleo hayawezi kupatikana na watu wa asili ndio wanataka hiyo amani, ndio wanayataka hayo maendeleo na, “kama tunachangia katika hilo, basi tupate manufaa.” Anasema.  

Je,ni kwa namna gani mikutano hii ya Umoja wa Mataifa imeisaidia jamii yake ya Watwa? Bwana Bambanze anasema, “kwanza ni kule kuwatambua watu wa asili kwamba wapo na wana haki zao na matatizo yanayowakabili yanaweza kujulikana na hapo kama matatizo yamejulikana, watu mbalimbali watoe michango ya kutimiza hizo haki na kuwasaidia watoke katika huo umaskini.”