Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru Burundi kwa haki za jamii ya Watwa

Vital Bambanze (kulia) mwakilishi wa jamii ya watwa nchini Burundi akiwa kwenye majadiliano na washiriki wengine wakati wa mkutano wa 21 wa jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la watu wa asili, UNPFII mwezi Aprili 2022 jijini New York, Marekani.
UN/ Flora Nducha
Vital Bambanze (kulia) mwakilishi wa jamii ya watwa nchini Burundi akiwa kwenye majadiliano na washiriki wengine wakati wa mkutano wa 21 wa jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la watu wa asili, UNPFII mwezi Aprili 2022 jijini New York, Marekani.

Nuru Burundi kwa haki za jamii ya Watwa

Haki za binadamu

Mkutano wa 21 wa Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la watu wa asili, UNPFFII likiwa limeingia siku ya tatu kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York, Marekani, washiriki kutoka Burundi wameieleza Idhaa ya Kiswahili ya  Umoja wa Mataifa juu ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha haki za binadamu za jamii ya asili aina ya watwa zinazingatiwa.
 

Mwakilishi wa jamii ya watwa Vital Bambanze amesema hatua hizo ni pamoja na viongozi kutambua kuwa warundi wote wako sawa ikiwemo watu wa jamii ya watwa.

“Ndio maana kama Rais wetu akihutubia au akizungumza na viongozi mbalimbali anawaeleza kuwa kama kuna watwa wako na matatizo mbalimbali, hakuna mtu mwingine kutoka nchi nyingine wa kuleta njia nzuri ya  kutatua matatizo hayo bali warundi. Hii inaonesha kuwa yeye ni mfano mzuri wa kiongozi na ni njia nzuri ya kupitia kwa watwa ili haki zetu zipate kutimizwa.

Amesema iwapo watwa au jamii yoyote ikibakia au ikiachwa nyuma, au kutelekezwa, inaweza kuleta madhara.

“Hivi sasa Burundi imeanza kuandika Mpango Mkakati wa kutatua matatizo ya watwa ,na tena tuna viongozi mbalimbali katika nyanja zinazoongoza nchi. Tuna Waziri wa Masuala ya Haki za Binadamu  kutoka jamii ya watwa, tuna wabunge na maseneta na watu mbalimbali wanaotusimamia. Hii yote inaonesha Burundi iko katika njia ya amani ya kutatua matatizo ya awali na tuko tunasonga mbele bila kumwacha mtu yeyote nyuma.”

Suala la umiliki wa ardhi kwa watwa uko vipi?

Kuhusu ardhi, Bwana Bambanze amesema takribani asilimia 65 ya watwa hawana ardhi na Burundi wakazi wake ni wafugaji na wakulima.

“Iwapo watwa hawana ardhi ya kutosha, wanakuwa hawawezi kupata chakula cha kutosha, hawaewzi kusomesha watoto, hawawezi kujipatia matibabu kwa sababu hawana mazao ya kutosha kuuza au mifugo. Hii inaleta tatizo la kunyanyaswa au kutumikia watu wengine ili walipwe fedha kidogo kidogo. Hii inaleta tatizo la kutokuwa na watu waliosoma ili watusimamie mambo mbalimbali nchini.” 

Amesema tatizo la ardhi linaleta matatizo yote yanayokabili watwa. 

Pontien Hatungimana, Afisa kutoka Wizara ya Mshikamano wa Kitaifa, Haki za Binadamu na Jinsia nchini Burundi akiwa kwenye mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani kando mwa mkutano wa 21 wa jukwaa la kudumu la Umoja w
UN/ Assumpta Massoi
Pontien Hatungimana, Afisa kutoka Wizara ya Mshikamano wa Kitaifa, Haki za Binadamu na Jinsia nchini Burundi akiwa kwenye mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani kando mwa mkutano wa 21 wa jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la watu wa jamii ya asili.

Je serikali inachukua hatua?

Akijibu hoja hiyo ya changamoto zinazokumba jamii ya watwa, Pontien Hatungimana, Afisa kutoka Wizara ya Mshikamano wa Kitaifa, Masuala ya Kijamii, Haki za Binadamu na Jinsia amesema hivi sasa mambo ni shwari kwa kuwa watwa wako serikalini, kwenye Seneti na Bungeni. Lakini hatua zinachukuliwa ili idadi yao iongezeke kwenye taasisi hizo.

Wana changamoto lakini tunachukua hatua- Hatungimana

“Lakini siwezi kusema hawana changamoto. Kuna tatizo la kukosa mashamba, watoto hawasomi, mambo ya afya na makazi bora” amesema Bwana Hatungimana.

Ameongeza kuwa “sasa hivi tuko kwenye kazi kubwa kuona hawa watu wanaishi vizuri. Tumeshaanda mpango wa serikali ili waishi kama warundi wengine. Kuna kazi tumefanya. Kuna watoto wako shuleni na serikali itawalipia fedha. Kuna watu wamepatiwa mashamba na wengine wamepatiwa kadi za afya.”

Bwana Hatungimana amesema pia kuna vyama vya ushirika na wanashawishi watwa waweze kujiunga na kushiriki.

Taswira katika ukumbi wa Baraza Kuu la UN wakati wa ufunguzi wa jukwaa la kudumu la UN la watu wa jamii ya asili, UNPFII
UN/ Manuel Elias
Taswira katika ukumbi wa Baraza Kuu la UN wakati wa ufunguzi wa jukwaa la kudumu la UN la watu wa jamii ya asili, UNPFII

Kuhusu UNPFII

UNPFII ni chombo cha ngazi ya juu cha ushauri kwa Baraza la Umoja wa Mataifa la kiuchumi na kijamii, ECOSOC.
Jukwaa hili lilianzishwa tarehe 28 mwezi Julai mwaka 2000 kupitia azimio namba 2000/22 la ECOSOC likiwa na mamlaka ya kushguhulikia masuala yote ya maendeleo kwa watu wa jamii ya asili, utamaduni, mazingira, elimu, afya na haki za binadamu.
Mkutano wa kwanza wa jukwaa hilo ulifanyika mwezi Mei mwaka 2022, na baada ya hapo kikao hufanyika kila mwaka kwa siku 10 kwenye makao makuu ya  Umoja wa Mataifa jijini  New York, Marekani.
Jukwaa linaweza kufanyika kwenye ofisi kuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi au kwingineko ikiridhiwa.