Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi twafanya uchaguzi mwakani, tuungeni mkono- Waziri Nibigira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, (kulia) akiwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Burundi  Ezéchiel Nibigira  baada ya mazungumzo yao jijini New York, Marekani
Picha ya UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, (kulia) akiwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Burundi Ezéchiel Nibigira baada ya mazungumzo yao jijini New York, Marekani

Burundi twafanya uchaguzi mwakani, tuungeni mkono- Waziri Nibigira

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Ezechiel Nibigira ameiambia Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa anakusudia baadaye hii leo kuuleza mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74 pamoja na mambo mengine, kuhusu hatua za maendeleo ambazo Burundi imepiga na pia kuiomba jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono nchi yake.

Waziri Nibigira anaanza kwa kueleza hali ilivyo hivi sasa nchini Burundi,

(Sauti ya Nibigira)

“Tumefika hapa ili tuujulishe ulimwengu hali halisi iliyoko Burundi. Nataka niuambie ulimwengu kuwa Burundi kuna amani ya kutosha. Burundi watu wanafanya kazi zao kwa utulivu. Burundi watu wanaenda kulima, wanaenda kwenye kazi mbalimbali, hakuna shida Burundi.”

Na baada ya hapo Waziri Nibigira anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono Burundi inapojiandaa na uchaguzi mkuu mapema mwakani,

(Sauti ya Nibigira)

“Kutokana na hiyo amani tuliyonayo leo, tuko tunajitayarisha kuingia katika uchaguzi mwaka ujao. Kutoka leo kuna miezi takribani 7 ili tuingie katika uchaguzi na tunajua kuwa uchaguzi huu utakuwa uchaguzi mzuri kuliko uchaguzi mwingine wowote ambao tumewahi kuwa nao hapo Burundi. Tunaomba ulimwengu wote uendelee kuwa na Burundi ili mafanikio ambayo tunayo hivi sasa Burundi, tuendelee kuwa mayo hata kesho na muda wote ujao.”