Teknolojia za watu wa asili kumulikwa wakati wa jukwaa lao New York

22 Aprili 2019

Mkutano wa jukwaa la kudumu kuhusu masuala ya watu wa asili unaanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ukileta pamoja zaidi ya watu 1,000 wa  jamii ya watu asili kutoka kona mbalimbali duniani.

Dkt. Elifuraha Laltaika, ambaye amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa jopo la wataalamu huru wa jukwaa hilo akiwasilisha Afrika tayari yuko New York Marekani na amezungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na hapa anafafanua kwa kina kile watakachoangazia akisema, “mwaka huu tunajikita katika maarifa ya asili. Na katika kuchakata maarifa ya asili tunaangazia namna ambavyo yanawasilishwa na kurithishwa kwa kizazi kimoja hadi kingine. Na ukingalia hiyo ni muhimu sana kwasababu mwaka huu Umoja wa Mataifa umeamua uwe mwaka wa lugha za asili na sisi tunaamini kwamba maarifa ya asili yanategemea sana uelewa wa zile lugha za asili kama moja  ya namna ya kurithisha lakini pia ya kuwasilisha yale maarifa ya asili,”

Alipoulizwa ni kwa nini  basi wamejikita kwenye teknolojia za asili, Dkt. Laltaika amesema, “tunaangalia sasa teknolojia itaboreshwa namna gani ili isiathiri maarifa ya asili lakini iongeze thamani au ladha katika kurithisha maarifa hayo. Kwa hiyo ni kitu cha muhimu sana kuangalia je teknolojia itaathiri au itaboresha maarifa ya asili na tangu mwaka jana tulishaamua kuwa mustakabali wa jamii unategemea sana, nyanja tofauti tofauti ikiwemo pia ya  uvumbuzi hata ya madawa na kadhalika na kadhalika.

Kando mwa maudhui hayo makuu, jukwaa hilo pia litajadili mwaka huu wa 2019 ambao ni mwaka wa kimataifa wa watu wa asili sambamba na ajenda ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa haki za watu wa jamii ya asili.

Dkt. Elifuraha Laltaika, mtaalamu wa jukwaa la kudumu la watu wa asili la Umoja wa Mataifa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili
UN News
Dkt. Elifuraha Laltaika, mtaalamu wa jukwaa la kudumu la watu wa asili la Umoja wa Mataifa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili

Ufunguzi wa Jukwaa

Mkutano huo wa 18 wa jukwaa la kudumu la kujadili masuala ya asili lilifunguliwa na tukio maalum la watoto wa kike wa taifa la Onondaga hapa Marekani na kufuatiwa na hotuba ya makaribisho kutoka kwa Chifu wa kabila hilo Tadodaho Sid Hill.

Kisha Makamu Rais wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, Valentin Rybakov, alihutubia akieleza kuwa ushauri wa wataalamu kutoka  jukwaa hilo unachangia katika maamuzi yanayopitishwa na Baraza hilo.

Kwa mantiki hiyo amesema, “hii ni muhimu sana na itasaidia sisi kufuatilia kwa kina utekelezaji wa ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.”

Ametaja hatua muhimu za kusaidia kufanikisha SDGs ikiwemo mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi kuhusu malengo hayo utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu sambamba na jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa litakalofanyika mwezi Julai kutathmini malengo 6 ya maendeleo endelevu, ikiwemo, elimu bora, ukuaji uchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mada hizi ni muhimu sana kwa watu wa jamii za asili na katika kufanikisha haki zao,” amesema Bwana Rybakoc akisisitiza kwa jukwaa hili la kudumu sambamba na hatua zinazofuatia ni za muhimu sana.

Amesisitiza pia umuhimu wa siyo tu kutambua haki za watu wa asili bali pia chanzo cha maarifa yao ya asili, umiliki na uhifadhi wa maarifa hayo.

Washiriki kwenye ufunguzi wa  mkutano wa 18 wa Jukwaa la kudumu la kujadili masuala ya watu wa asili.
UN /Loey Felipe
Washiriki kwenye ufunguzi wa mkutano wa 18 wa Jukwaa la kudumu la kujadili masuala ya watu wa asili.

Maarifa ya asili ni dhahiri

Mada ikiwa ni teknolojia na maarifa ya asili, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa kimataifa wa kuhifadhi bayonuai Cristiana Pasca Palma, amemwagia sifa mababu zake wa kiroma ambao amesema walikuwa wakitumia mbinu za kijadi za kilimo ambazo zilirithishwa kutoka kizazi na kizazi.

Mbinu hizo ni pamoja na jinsi ya kulima bila kuharibu bayonuia akisema , “mababu na mabibi zetu sote wamekuwa wakitegemea ardhi na maji kwa njia moja au nyingine na maarifa yao ya asili ambayo mara nyingine yalirithishwa kupitia wanawake; kutoka kwa bibi kwenda kwa mama na mtoto, yametuwezesha sisi kustawi kwa miaka 1000.”

Jukwaa la kujadili masuala ya jamii ya watu wa asili lilianzishwa na ECOSOC mwaka 2000 na lengo lake ni kutoa ushauri kuhusu masuala ya watu wa asili.  Jukwaa hilo lina wataalamu huru 16 ambao 8 kati yao wamechaguliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifana 8 wamechaguliwa na mashirika ya kimataifa yanayohusika na masuala ya watu wa asili.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter