Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha tano cha UNEA chafungua pazia:UNEP

Ekari kadhaa za msitu wa Amazon zimetiwa moto ili kupitisha mashamba ya miwa na maharagwe ya soya bila kujali madhara kwa mazingira.
UNEP GRID Arendal/Riccardo Pravettoni
Ekari kadhaa za msitu wa Amazon zimetiwa moto ili kupitisha mashamba ya miwa na maharagwe ya soya bila kujali madhara kwa mazingira.

Kikao cha tano cha UNEA chafungua pazia:UNEP

Tabianchi na mazingira

Kikao cha tano cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa , UNEA leo kimefungua pazia jijini Nairobi Kenya ambapo kimewaleta pamoja nchi wanachama, wanaharakati na wadau wa mazingira kwa njia ya mtandao kujadili masuala mbalimbali ya mazingira na maendeleo endelevu.

Lengo la kikao hicho ni kuimarisha juhudi za kushughulikia mazingira kweye muktadha wa maendeleo endelevu, na kutoa kipaumbele kwa utekelezaji wake kikamilifu. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP, kikao hiki cha tano cha UNEA mwaka 2021 kinatumiwa kama jukwaa la kuhamasisha, kuchagiza na kuzitia moyo nchi wanachama na wadau mbalimbali kushiriki na kutekeleza mbinu muafaka na suluhu zitokanazo na mazingira yatakayochangia kufikia ajenda yam waka 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs hasa katika kutokomeza umaskini na kubuni mbinu endelevu za uzalishaji na matumizi ya bidhaa.

Mabadilko ya tabianchi yanaathiri nchi nyingi ikiwemo Fiji iliyokumbwa na kimbunga mwaka 2016.
OCHA/Danielle Parry
Mabadilko ya tabianchi yanaathiri nchi nyingi ikiwemo Fiji iliyokumbwa na kimbunga mwaka 2016.

Mbinu za kudhibiti mazingira zibadilike

Katika ufunguzi wa Baraza hilo mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen amese kuwa hatua za kudhibiti mazingira hivi sasa lazima zibadilike. 

“Hii ni kwa sababu changamoto za sasa ni kubwa mno na hasa changamoto zitokanazo na COVID-19. Lazima tufanye biashara, uwekezaji  na kurejea katika maelewano na mazingira asilia. Hii ina maana kuunga mkono ukwamukaji wa kiuchumi usioharibu mazingira kutoka katika janga la Corona,” amesema Bi, Andersen. 

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa video kwenye mkutano huo amesema serikali zote na watu wake wanahitaji kutambua katika vinasaba vyao kwamba changamoto zote za mazingira, kijamii na kiuchumi zinahusiana na zinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja.

Mathalani amesema ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu yam waka 2030 “Tunahitaji kuzuia kusambaratika kwa mfumo wa maisha ambao utaathiri uhakika wa chakula na maji kote ulimwenguni.”

Mataifa ya Kusini na Mashariki mwa Afrika yanaendelea kukabiliwa na mafuriko, ukame na matukio mengine ya mabadiliko ya hali ya hewa katika miaka ya karibuni
UNDP/Arjen van de Merwe
Mataifa ya Kusini na Mashariki mwa Afrika yanaendelea kukabiliwa na mafuriko, ukame na matukio mengine ya mabadiliko ya hali ya hewa katika miaka ya karibuni

Ameongeza kuwa hivi sasa dunia nzima iko katika mgogoro “Bahari zimejaa plastiki na zinakuwa na tindikali, dunia inaelekea kwenje kubwa la joto la kupindukia la zaidi ya nyuzi joto 3 na bayoanuai inapungua kwa kasi ya juu.

Amesisitiza kwamba “Hatuna chaguo bali ni kubadili jinsi gani uchumi wetu na jamii zetu zinavyothamini mazingira na maliasili. Ni lazima tutoe kipaumbele katika afya ya sayari katika mipango yetu yote na sera.”

Ameongeza kuwa masuala ya uchumi yako bayana, zaidi ya nusu ya pato la taifa linategemea maliasili lakini mtaji wetu wa asili umeshuka kwa asilimia 40 kwa kipindi cha miongo miwili.

Na ndio maana jukwa la kiuchumi la dunia limeorodhesha kupotea kwa bayoanuai na kusambaratika kwa mfumo wa Maisha kama moja ya matishio matano mwakubwa ambayo yataukabili ubinadamu katika miaka 10 ijayo na hivyo uharaka wa kuchukua hatua sasa uko bayana.

Barafu ikielea juu ya maji katika eneo la Prince Gustav Antarctica
WMO/Gonzalo Javier Bertolotto Quintana
Barafu ikielea juu ya maji katika eneo la Prince Gustav Antarctica

Maudhui yam waka huu

Maudhi ya mwaka huu ni uimarishaji juhudi za kushughulikia mazingira ili Kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kaulimbiu hii inatoa wito wa kuimarisha juhudi za kushughulikia na kuboresha mazingira na kutoa suluhu inayotokana na mazingira ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu kupitia vipengele vyake vitatu vinavyohusiana vya (kijamii, uchumi na mazingira).  

Kaulimbiu mbiu hii ilikubaliwa wakati wa mkutano uliojumuisha Baraza la utawala na kamati ya mabalozi wa Kudumu uliofanyikam tarehe 3 Disemba mwaka wa 2019, baada ya majadiliano ya kina na nchi wanachama na wadau wakiongozwa na Bw. Fernando Coimbra, mwenyekiti wa kamati ya mabalozi wa kudumu, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Brazil nchini Kenya, na Bi. Elin Bergithe Rognlie, Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Norway nchini Kenya.