Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu wa mazingira unahatarisha afya za binadamu-UNEP

Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.
NASA
Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

Uharibifu wa mazingira unahatarisha afya za binadamu-UNEP

Tabianchi na mazingira

Uharibifu wa sayari dunia ni mkubwa sana na afya za wakazi wa dunia hiyo zipo hatarini iwapo hatua hazitachukuliwa hivi sasa, imesema ripoti ya hali ya mazingira iliyotolewa hii leo na shrika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa kufuatia utafiti wa mazingira kwa kipindi cha miaka mitano ni kazi ya wanasayansi 250 na wataalam kutoka takriban nchi 70 na inasema kuwa iwapo hatua za haraka za kulinda mazingira au miji hazitachukuliwa, ifikapo katikati ya karne hii, maeneo kama vile ya Asia, Mashariki ya kati na Afrika yatashuhudia watu wake wakifariki dunia mapema vifo.

Aidha ripoti hiyo inaonya kuwa vichafuzi katika maji yasiyo ya chumvi vitakuwa sugu dhidi ya dawa za vijiua viumbemaradhi na kuwa sababu kuu ya vifo ifikapo mwaka 2050 huku baadhi ya kemikali zitaathiri uwezo wa kuzaa miongoni mwa wanawake na wanume na ukuaji wa neva wa mtoto.

Hata hivyo ripoti hiyo imetaja kwamba dunia inayo teknoloji, sayansi na fedha zinazohitaji ili kusongesha maendeleo endelevu licha ya kwamba msaada unahitajika kutoka kwa viongozi wa umma, biashara na siasa ambao bado wanashikilia uzalishaji kupitia mifumo ya zamani unahitajika.

Ripoti hiyo ya sita ya mtazamo wa mazingira kimataifa imetolewa wakati huu ambapo mawaziri kutoka kote ulimwenguni wamekutana mjini Nairobi Kenya kushirki katika Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa.

Baraza hilo linalenga kuangazia maswali muhimu ikiwemo mbinu za kukabiliana na uharibifu wa chakula, kuchagiza kuhusu magari yanayotumia kawi ya umeme na kukabiliana na jamga la uchafuzi wa platiki katika mabahari ikiwemo changamoto zingine.

Akizungumzia ripoti hiyo kaimu Mkurugenzi Mkuu wa UNEP, Joyce Msuya amesema, “sayansi iko wazi na kwamba ustawi wa kiafya wa binadamu unahusiana moja kwa moja na hali ya mazingira yetu.”

Ameongeza kuwa, “ripoti hii ni mtazamo kwa binadamu, tuko njia panda, je tuendelee katika barabara tuliyopo ambayo itaishia kwenye mustakabali usio bora kwa binadamu au tuchukue hatua na kusonga katika njia ambayo ni endelevu? Haya ndio maamuzi wanayohitaji kufanya viongozi wetu wa kisiasa.”

Utupaji hovyo wa chakula ni adui mkubwa wa vita dhidi ya njaa
FAO/Jonathan Bloom
Utupaji hovyo wa chakula ni adui mkubwa wa vita dhidi ya njaa

Chaguo la sera bunifu

Kwa mujibu wa ripoti, mustakabali wa watu wenye afya unaendana na fikra tofauti ambapo mfumo wa ‘zalisha sasa, safisha baadaye,’ unabadilishwa na kuwa uchumi wa uharibifu sifuri ifikapo mwaka 2050 ambapo kwa mujibu wa makadirio uwekezaji wa asilimia 2 wa pato la taifa utasababisha ukuaji wa muda mrefu kwa viwango vilivyotarbiriwa lakini na athari ndogo zaidi kwa mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa maji na uharibifu wa mazinigira.

UNEP kupitia ripoti hiyo imesema, dunia haiko katika mwelekeo wa kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 au 205o na kwamba hatua za haraka zinahitajika kwani kupungua kwa kasi huenda kukaathiri ufikiaji wa malengo ya makubaliano ya mkataba wa Paris au kurudisha nyuma hatua zilizopigwa

Kwa mantiki hiyo ripoti imependekeza kula mlo ulio na bidhaa chache za nyama, kupunguza uharibifu wa vyakula katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea ambavyo vitapunguza haja ya kuzalisha chakula kwa asilimia 50 kwa ajili ya kulisha watu takriban bilioni 9 hadi 10 wanaokadiriwa kuwa duniani ifikapo mwaka 2050. Aidha ripoti imetoa wito kukabiliana na uchafuzi wa platiki tani milioni 8 zinazoishia baharini kila mwaka.

Ripoti inataka uwepo wa será zinazopatia majibu mifumo yote kama vile nishati, chakula na taka badala ya será zinazolenga kitu kimoja kimoja ikitolea mfano kuwa tabianchi imara na hewa safi vinashabiana na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mkataba wa Paris huenda zitagharimu dola trilioni 22, lakini faida za kiafya zitokanzo na kupunuga kwa uchafuzi wa hewa huenda kukazalisha dola trilioni 54 za ziada.