Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usawa katika mgao wa chanjo ya COVID-19 ni tishio la kutokomeza ugonjwa huo- Guterres

Mtu wa kujitolea apokea chanjo dhidi ya COVID-19 ya AstraZeneca nchini Uingereza.
University of Oxford/John Cairns
Mtu wa kujitolea apokea chanjo dhidi ya COVID-19 ya AstraZeneca nchini Uingereza.

Ukosefu wa usawa katika mgao wa chanjo ya COVID-19 ni tishio la kutokomeza ugonjwa huo- Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema ukosefu wa uwiano katika mgao na utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona, au COVID-19 ni tishio kubwa katika kutokomeza ugonjwa huo ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu milioni mbili duniani kote.

Guterres amesema kupatikana kwa chanjo kumethibitisha umuhimu wa sayansi kuliko wakati wowote na usambazaji wa chanjo hizo umeanza kuleta matumaini.

“Ni nchi 10 tu zimesambaza asilimia 75 ya chanjo zote za COVID-19. Wakati huo huo zaidi ya nchi 130 hazijapokea hata dozi moja. Nchi ambazo zinakumbwa na mizozo na ukosefu wa usalama ziko hatarini zaidi kuachwa nyuma. Janga linapopiga, tutakuwa sote salama pindi kila mtu anapokuwa salama,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa iwapo virusi vya Corona vitaachiwa visambae kama moto wa nyika katika nchi za kusini, au katika baadhi ya nchi hizo, “virusi hivyo vitabadilika zaidi. Aina mpya ya virusi itakuwa rahisi zaidi kusambaa, hatari zaidi na kutishia hata ufanisi wa chanjo za sasa.”

Bwana Guterres amesema hali hiyo itasababisha virusi kurejea kwa nguvu zaidi katika nchi zilizoendelea na kuleta madhara zaidi.

Lazima tuhakikishe kila mtu, kila mahali anaweza kupata chanjo haraka iwezekanavyo kwa kuwa kinyume cha hapo hata harakati za kukwamua uchumi wa dunia zitadorora.

Mfanyakazi nchini India ambaye anataka kupata chanjo dhidi ya COVID-19.
UNICEF India/ Ruhani Kaur
Mfanyakazi nchini India ambaye anataka kupata chanjo dhidi ya COVID-19.

Umuhimu wa COVAX

Akizungumzia mfumo wa kimataifa COVAX wa kununua na kusambaza chanjo dhidi ya Corona kwa nchi za kipato cha kati na cha chini, Katibu Mkuu amesema mfumo huo unahitaji kufadhiliwa na zaidi ya hapo harakati zake lazima ziratibiwe.

“Dunia inahitaji kwa udharura mpango wa kimataifa wa utoaji chanjo utakaoleta pamoja wale wenye uwezo, utaalamu wa kisayansi na uwezo wa kuzalisha na uwezo wa kifedha. Naamini kundi la nchi 20 au G20 lina uwezo wa kuanzisha kikosi kazi cha dharura kuandaa mpango huo na kuratibu utekelezaji na ufadhili wake,” amesema Guterres.

Amesema kikosi kazi hicho kinapaswa kujumuisha nchi zote ambamo kwazo  zina uwezo wa kutengeneza au kuzalisha chanjo iwapo leseni zinaruhusu pamoja na taasisi zingine kama shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, ubia wa chanjo duniani, GAVI na taasisi nyingine za kimataifa za kifedha na kiufundi.
 
Bwana Guterres amesema kwa upande wake yeye yuko tayari kuhamasisha uungwaji mkono wa jitihada hizo kutoka Umoja wa Mataifa akisema kuwa, “katika mkutano wa baadaye wiki hii wa kundi la nchi 7 au G7 unaweza kuweka kasi ya kuhamasisha upatikanaji wa fedha.”

Amesisitiza kuwa kwa pamoja dunia inaweza kuhakikisha upatikanaji, usambazaji wa chanjo hiyo kwa haki na imani ya watu kwa chanjo husika.
 
“Tunaweza kushinda ugonjwa, tunaweza kuibua uchumi wa dunia na ninashawishika kuwa inawezekana, hebu na tufanye hivyo kwa pamoja,” amesema Katibu Mkuu.

Sitisho la mapigano

Katika mkutano wake huo,  Katibu Mkuu ameishukuru Uingereza kwa kuandaa mkutano wa leo na kwa kuendelea kusisitiza wito wake wa sitisho la mapigano duniani, kuandaa fursa ya diplomasia na kuwezesha huduma za kibinadamu ikiwemo kuwezesha usambazaji wa chanjo duniani kote.