
Virusi vilivyotikisa dunia: 2020, mwaka tofauti na mingine
Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona au COVID-19 uko kila pahali na katika mwaka 2020 ulisambaa na kuleta madhara makubwa yaliyosababisha janga la dunia ambalo mapana yake hayakutarajiwa. Katika mfululizo wa makala sita juu ya mwaka huu wa mtikisiko, UN News inamulika athari za ugonjwa huu kwa watu kwenye maeneo mbalimbali ya dunia na suluhisho ambazo Umoja wa Mataifa umependekeza kufuatia janga hili. Katika makala hii ya kwanza tunamulika mambo ya msingi katika miezi 12 ya mwaka huu wa 2020.

Mwaka 2020 unavyofunga pazia, na watu kila kona ya dunia wakitathmini jinsi ambavyo dunia imebadilika, wanakabiliwa na takwimu za kutisha. Idadi ya watu ambao wamekufa baada ya kuambukizwa COVID-19 inanyemelea milioni mbili.

Mapema mwaka huu, safari za kimataifa zilikumbwa na vikwazo vikubwa, watu kama wasafiri hawa nchini Thailand walitambua umuhimu wa kuvaa vazi la kujikinga mwili mzima, PPE, vazi ambalo sasa limejipatia umaarufu duniani.

Punde, hofu ilitanda kuhusu uhaba wa mavazi hayo, PPE, na Umoja wa Mataifa ulisaidia nchi kadhaa katika ununuzi wa vifaa hivyo ikiwemo China ambako virusi hivyo vilianzia.

Kadri COVID-19 ilivyozidi kushika kasi, nchi na maji nayo duniani kote ilianza kuweka vikwazo vya matembezi, shule zikafungwa, shughuli za michezo na kitamaduni halikadhalika bila kusahau biashara ambazo zilionekana kuwa hazina umuhimu.

Kwa kawaida, miji yenye kukurukakara nyingi kama vile mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ulikuwa kimya kwa kuwa watu walilazimika kusalia majumbani.

Umoja wa Mataifa ulisalia wazi ukiendelea na majukumu yake duniani kote, ijapokuwa matukio muhimu kama vile mkutano wa kila mwaka wa mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu New York, Marekani ulifanyika kwa njia tofauti. Ni wajumbe wachache tu ambao waliruhusiwa kuingia kwenye vyumba vya mkutano huku marais na viongozi wakuu wa nchi wakihutubia kwa njia ya mtandao.

Dunia kote watu walianza sasa kuzingatia kanuni mpya za kutochangamana, kuhakikisha umbali wa futi 6 kati ya mtu na mtu iwe shuleni, madukani au kwingineko kwenye huduma. …..

…na watu walikumbushwa kuhusu umuhimu wa kunawa mikono kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya magonjwa.

Wanafunzi ambao hawakuweza kwenda shule, walilazimika kuzoea ukweli mpya wa jinsi ya kuendelea na masomo yao wakiwa nyumbani.

Wakati Afrika ilionekana kutopata madhara makubwa kutokana na virusi vya Corona ikilinganishwa na mabara mengine, kwa kuzingatia idadi ya maambukizi na vifo, Umoja wa Mataifa ulipaza sauti kuwa gonjwa hilo litatumbukiza watu wengi zaidi kwenye umaskini.

Jambo muhimu zaidi ni kwamba Umoja wa Mataifa ulikuwa unasaidia wakimbizi na makundi mengine yanayohamahama na yaliyo hatarini zaidi kama vile maelfu ya wakimbizi warohingya kutoka Myanmar waliosaka hifadhi kwenye mpaka na Bangladesh.

Hadi sasa kuna maendeleo yamepatikana, katika rekodi ya aina yake, wanasayanasi wametengeneza chanjo fanisi dhidi ya COVID-19 na ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, watu walishaanza kupatiwa chanjo hiyo katika nchi zilizoendelea.

Dunia inapoingia mwaka 2021, janga la Corona bado linatikisa, na baada ya angalau nusu mwaka ya ukimya, bado maambukizi na vifo vinaripotiwa. Jinsi chanjo zaidi zinavyozidi kutengenezwa, jamii ya kimataifa inaombwa kushirikiana ili kuepusha kusambaa zaidi kwa virusi hivyo na kufuata miongozo ya kisayansi.
Kwa taswira zaidi ya mwaka 2020, endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi maalum kadi mwaka unavyoyoyoma.