Kuna hatua zimepigwa Maziwa makuu lakini bado kuna kibarua kufikia amani ya kudumu:Xia

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu Huang Xia ameliambia Baraza la Usalama kuhusu umuhimu wa "kulinda mafanikio yaliyopatikana huku wakishughulikia kwa bidii changamoto zinazoendelea" katika eneo hilo.
Katika hotuba yake kwenye Baraza hilo leo, Xia amesema Ukanda wa Maziwa Makuu umeshuhudia kuimarika kwa uhusiano wa nchi mbili na kusababisha kufufuliwa kwa mifumo ya ushirikiano katika nyanja ambalimbali ikiwa ni pamoja na usalama, biashara, miundombinu, uchukuzi, maliasili na nishati.
Mjumbe huyo amekaribisha maendeleo yaliyopatikana katika eneo la ushirikiano wa usalama kwa lengo la kupambana na vikundi vyenye silaha Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mjumbe Maalum amesema kuzinduliwa kwa Kikundi cha mawasiliano na uratibu, ambacho kinatoa motisha isiyo ya kijeshi kwa vikundi vyenye silaha kupokonywa silaha zao, pia ni jambo muhimu la juhudi hizi katika ngazi ya kikanda.
Licha ya mafanikio haya amesema Bwana Xia changamoto bado zipo. Amesema shughuli zinazoendelea za vikundi vyenye silaha bado ni tishio kubwa kwa amani na utulivu katika eneo hilo, na kuongezeka kwa mashambulio, yakiwemo yanayofanywa na kundi la ADF mashariki mwa DRC au yale yaliyozinduliwa na RED-Tabara dhidi ya uwanja wa ndege wa Bujumbura mwezi Septemba.
Xia ameongeza kuwa, "Vurugu hizi zinaendelea kuwa na athari mbaya kwa hali dhaifu ya kibinadamu, na pia juu ya utulivu wa kijamii na kiuchumi wa maeneo yaliyoathiriwa. Vikosi vya waasi pia vinaendelea kushiriki katika unyanyasaji na biashara haramu ya maliasili ambayo mapato yake yanagharimia usambazaji wa silaha na ajira zao."
Mjumbe huyo Maalum amesema janga la COVID-19 pia, kwa kiwango fulani, limeongeza udhaifu wa kijamii na kiuchumi uliokuwepo awali.
Kulingana na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, ni dozi milioni 36 tu za chanjo ambazo zimetolewa hadi sasa katika ukanda huo, ambao una idadi ya watu karibu milioni 450.
Xia amerejea ombi lililotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres la kutaka mshikamano zaidi na nchi zinazoendelea, ili kuwezesha upatikanaji wa chanjo na kuimarisha mifumo na miundombinu ya afya iliyopo.
Xia amesisitiza kuwa kukabiliana vyema na changamoto za eneo hilo, wakati akiunga mkono juhudi nzuri zinazoendelea, kutahitaji nguvu ya pamoja ya mataifa ya eneo hilo, asasi za kiraia, mashirika ya kikanda, washirika wa kimataifa, na Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa ukanda wa Maziwa Makuu hivi sasa uko njiapanda “Hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ni muhimu kuendeleza mafanikio yaliyopatikana huku tukishughulikia changamoto zinazoendelea. Na mafanikio ya mtazamo huo yanahitaji kujifunza kutokana na mambo yaliyopita na kuonyesha mshikamano wa kuwasaidia watu wa ukanda wa Maziwa Makuu katika kujenga leo na kesho yenye matumaini na amani.”
Katibu Mkuu msaidizi wa Umoja wa Mataifa barani Afrika Martha Pobee amesema Umoja wa Mataifa umechukua hatua za kurekebisha uwepo wake katika eneo hilo ili kushughulikia vyema changamoto zilizosalia za amani na usalama, haswa mashariki mwa DRC.
Amesema ukosefu wa usalama unaoendelea Mashariki mwa DRC bado ni moja ya changamoto kubwa zinazoukabili ukanda hu oleo hii.
Pobee ameongheza kuwa vikundi vya kitaifa na vya kigeni vyenye silaha vinaendelea kufanya kazi na kutekeleza mashambulio mabaya dhidi ya raia, na kuongeza kuzorota kwa hali mbaya ya kibinadamu.
Amebainisha kuwa mwaka huu wa 2021, angalau raia 1043 wameuawa, wakiwemo wanawake 233 na watoto 52.
Pobee amekumbusha kwamba operesheni za kijeshi zinapaswa kufanywa kwa kufuata kwa kuzingatia sera za haki za binadamu na kuhakikisha upunguzaji wa athari kwa raia ili kuepuka mateso kwa idadi kubwa ya watu wanaopaswa kulindwa.
Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu amekaribisha kupitishwa kwa mpango wa utekelezaji wa miaka mitatu wa kikundi cha mawasiliano na uratibu kinacholenga kudhoofisha nguvu za waasi kupitia njia isiyo ya kijeshi.
Amesema MONUSCO na ofisi ya mjumbe Maalum wataendelea kutoa msaada kwa utekelezwaji wa kundi hilo kupitia kuanzishwa kwa kitengo maalum cha utendaji ambacho kitasimamiwa huko Goma.