Ushirikiano wa kimataifa umeshindwa kukidhi haja wakati wa COVID-19:Guterres 

24 Septemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliambia Baraza la Usalama hii leo kwamba ushirikiano wa kimataifa umeiangusha dunia na kushindwa kukidhi haja wakati huu wa janga la corona au COVID-19 na hivyo ametoa wito wa kutafakari kwa kina kuhusu suala la utawala wa dunia na ushirikiano wa kimataifa. 

Guterres ameyasema hayo wakati wa kikao maalum cha Baraza la Usalama kilichojikita katika mada ya ya utawala wa dunia na uwezekano wa mabadiliko katika usalama wa kimataifa katika mazingira ya kujikwamua kutoka kwenye janga la COVID-19 na athari zake kinachofanyika kandoni mwa mjadala wa Baraza Kuu UNGA75 kunaoendelea mjini New York. 

“Janga la COVID-19 ni bayana kwamba limeweka ushirikiano wa kimataifa katika mtihani mkubwa , mtihani ambao tumeanguka. Virusi ambayo tayari vimeshakatili maisha ya watu karibu milioni moja na kuambukiza wengine zaidi ya milioni 30 kote duniani bado havijadhibitiwa. Hali hii imeletwa na ukosefu wa maandalizi, ushirikiano, umoja na mshikamano katika ngazi ya kimataifa.” 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa Yanatukumbusha ni yapia waasisi wetu waliyafikia na kutukaribisha kufuata nyazo za kutimiza malengo yao. Tunahitaji kufikiri haraka na kwa ubunifu kuhusu utawala wa dunia na ushirikiano wa kimataifa ili kuufanya uende sanjari na karne ya 21.” 

Mkutano huo umeendeshwa na Rais wa Niger Mahamadou Issoufou ambaye nchi yake ndiye Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Septemba. 

Mwenyekiti wa tume ya Muungano wa afrika (AU) Moussa Faki Mahamat pia ameshiriki mkutano huo. 

Guterres amesema dunia, “inahitaji mtandao wa ushirikiano wa kimataifa wenye misingi imara na ushirikiano baina ya mashirika ya kimataifa na kikanda, taasisi za kimataifa za fedha na wadau wengine wa kimataifa na taasisi.” 

Ushirika na Muungano wa Afrika (AU) 

Bwana Guterres ametolea mfano ushirikiano wa kimkakati wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika ambao aliufanya kuwa ni kiupaumbele. 

“Ushirikiano baina ya AU na Umoja wa Mataifa ni mfano ambao tunapaswa kuiga katika ushirika wet una mashirika mengine ya kikanda.” Amesema. 

Pia ametoa wito kwa Baraza la usalama kudumisha ushirikiano huu kwa kuanzisha uhusiano imara na rasmi na Baraza la AU la amani na Usalama na pia kufanya nalo mawasiliano mara kwa mara. 

“Hii itatoa mgawanyo wa kazi katika njia ambayo ni bora na yenye ufanisi zaidi . Muungano wa Ulaya unaweza kufanya uhimizaji wa amani na operesheni za kupambana na ugaidi, ambazo zitakuwa zikiungwa mkono na Baraza la Usalama na linaweza kufaidika na ufadhili, unaohakikishwa na michango ya lazima. “  

Amesisitiza Guterres na kuongeza kwamba, “hii ndio njia pekee ya kujenga ushirika tunaohitaji kupambana na ugaidi katika bara la afrika na kukamilisha mradi wa AU wa kunyamazisha silaha.”. 

Katibu Mkuu pia amesema kwamba Umoja wa Mataifa lazima uboreshe ufanisi wa michango yake katika utawala wa kimataifa. 

Kwa mtazamo wake wajibu mkuu wa kuhakikisha utendaji wa utawala wa kimataifa uko mikononi mwa nchi wanachama. 

“Mabadiliko katika utawala wa kimataifa sio mbadala kwa hatua za Pamoja za nchi wanachama kuweza kukabili changamoto za pamoja.” 

Ujumuishwaji wa wanawake na vijana 

 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba shirika na wanachama wake “hawako sambamba na hali halisi iliyoko duniani leo hii. Taasisi za utawala wa kimataifa ni lazima zifanyekazi pamoja katika uratibu maalum, zikidhibiti na kupunguza hatari za kila aina.” 

Amesisitiza kwamba haiwezekani kuendelea kuchukua hatua za papo kwa papo katika mfumo wa kimataifa na bila kutabiri hatari zijazo na kuzipatia suluhu. 

“Janga hili ni kengele ya majanga hata makubwa zaidi ambayo yatatokea kuanzia na changamoto ya mabadilio ya tabianchi. Endapo tutachukua hatua bila umoja na mpango maalum kama tulivyoshuhudia mwaka huu , nina hofu ya zahma mbaya zaidi. Tunahitaji utawala wa kimataifa ambao umedhamiria , wenye mpangilio na uliuo tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter