Baraza la Usalama lapitisha azimio kuunga mkono usitishwaji uhasama wakati wa COVID-19

1 Julai 2020

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limeunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa kutaka usitishwaji uhasama kote duniani , ili kukabiliana na janga la corona au COVID-19 ambako tayari limeshakatili Maisha ya watu zaidi ya nusu milioni.

 

Kupitia azimio namba 2532 la 2020 lililopitishwa kwa kauli moja bila kupingwa , wajumbe wote 15 wa chombo jicho katika ajenda yao wamedai “Usitishwaju wa uhasama kote na mara moja katika mizozo yote.”

Pia Baraza hilo limeelezea uungaji mkono wa juhudi za Katibu Mkuu António ambaye ndiye aliyetoa ombi kwa mara ya kwanza Machi 23 mwaka huu la kutaka usitishwaji uhasama mara moja kote duniani.

Kuhatarisha amani

Baraza hilo limesema kiwango kisichotarajiwa cha janga la corona kina uwezekano wa kuhatarisha udumijashi wa amani na usalama wa kimataifa na kuongeza kwamba pia kitarejesha nyuma hatua zilizopigwa katika ujenzi wa amani na maendeleo katika nchi zinazoibuka kutoka kwenye mizozo.

Azimio hilo la kurasa mbili lililoandaliwa na Ufaransa na Tunisia limepitishwa siku 111 baada ya shirika la afya duniani WHO kutangaza kwamba COVID-19 ni janga la kimataifa.

“Ni ishara nzito ya umoja ndani ya Baraza la Usalama na ishara ya matumaini ambayo tunaituma kutoka Baraza la Usalama kwenda duniani kote “ amesema Christoph Heusgen, mwakilishi wa kudumu wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa akitangaza kwamba wajumbe wote 15 wameunga mkono azimio hilo katika siku yake ya kwanza kama Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Julai.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wakikutana kwa njia ya video kuhusiana na mkakati wa Kimataifa wa Makosa ya Jinai.
UN Photo/Eskinder Debebe
Wajumbe wa Baraza la Usalama wakikutana kwa njia ya video kuhusiana na mkakati wa Kimataifa wa Makosa ya Jinai.

 

Kutoa fursa ya misaada ya kibinadamu

Kupitia azimio hilo Baraza limetoa wito kwa pande zote hasimu katika mizozo kujihusisha mara moja katika usitishwaji uhasama wa muda mrefu kwa ajili masuala ya misaada ya kibinadamu. Limetaka takribani usitishwaji vita kwa siku 90 ili kuruhusu usafirishaji salama, bila vikwazo na endelevu wa misaada ya kuokoa maisha.

Hata hivyo azimio hilo limesisitiza kwamba hakutakuwa usitshaji uhasama wowote kwa operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la ISIL linalojulikana pia kama Da’esh, Al Qaeda, kundi la Al Nusra Front na makundi mengine ambayo Baraza limeyaorodhesha kama ya kigaidi.

Pia azimio hilo limemuomba Katibu Mkuu kuzipa maagizo operesheni 13 za ulinzi wa amani kuzisaidia nchi husika katika juhudi za kukabiliana na janga la corona na kutoa taarifa mpya kuhusu juhudi za Umoja wa Mataifa za kushughulikia COVID-19 katika maeneo yenye vita na migogoro ya kibinadamu.

Azimio hilo la leo Jumatano halikutaja popote kuhusu shirika la afya duniani WHO. Katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa Jumanne idadi ya wagonjwa wa COVID-19 kote duniani sasa imefikia 10,185,374 na vifo 503,862.  Nchi zilizoathirika Zaidi ni za Amerika ambako jumla ya wagonjwa ni 5, 136,705 na vifo 247,129.

Maazimio ya Baraza la Usalama hivi sasa yanapitishwa kwa muundo wa kura ya maandishi  kutokana na utaratibu wa muda uliowekwa na wanachama wa Baraza hilo mwezi Machi kutokana na mlipuko wa janga la COVID-19.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter