Umoja, ubia na ushirikiano wa dhati ni muarobaini wa kutokomeza FGM
Umoja, ubia na ushirikiano wa dhati ni muarobaini wa kutokomeza FGM
Umoja wa Mataifa umetaka ushirikiano katika ngazi zote na katika sekta zote za kijamii ili kulinda mamilioni ya wasichana na wanawake walio hatarini kukumbwa na ukeketeaji (FGM) kila mwaka.
Umuhimu wa ushirikiano huo umeonekana dhahiri zaidi hivi sasa kwa hofu kuwa ukeketaji wa watoto wa kike na wanawake milioni mbili unaweza kufanyika katika muongo ujao wakati huu ambapo janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limesababisha shule kufungwa na kuvuruga mipango mingine ya ulinzi wa kundi hilo dhidi ya FGM.
Katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameangazia kuwa kwa kushirikiana “kwa pamoja tunaweza kutokomeza FGM ifikapo mwaka 2030.”
“Wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unaingia katika muongo wa hatua za utekelezaji wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, hebu na tuufanye muongo huu kuwa muongo wa kutokuwepo kwa vitendo vya ukeketaji,” amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema kwa kufanya hivyo dunia itavuna mafanikio chanya kwenye afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake na watoto wa kike.
Usawa jinsia na kutokomeza FGM vinaenda pamoja
Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la idadi ya watu, UNFP nao pia wamesema kuwa kutokomeza ukeketaji watoto wa kike na wanawake na kufanikisha usawa wa jinsia ni mambo mawili yanayoimarisha malengo ya SDGs.
“Hebu weka tu kwamba usawa wa jinsia ungalikuwa ni kitu kipo, kusingalikuwepo na FGM. Hii ni dunia tuitakayo,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore na Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Natalia Kanem katika taarifa yao ya pamoja.
Wametaka ushirikiano thabiti na Umoja katika ngazi zote na sekta zote sambamba na upatikanaji wa fedha za kutosha ili kulinda na kunusuru wanawake na wasichana walio hatarini kukeketwa.
“Tunafahmau kile kinachowezekana. Tumevumilia visingizio. Tumechoshwa na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Ni wakati wa kuungana kupitia mikakati iliyoidhinishwa, tuipatia ufadhili wa kutosha na tuchukue hatua,” wamesisitiza.
Mila potofu na dhalili
FGM ni kitendo hatari, dhalili na kinachukia ambacho ni sawa na ukiukwaji wa haki za binadamu. Kitendo hiki kinahusisha kuondoa sehemu au kuondoa kabisa eneo la siri la mwanamke bila sababu zozote za kitabibu. Katika tamaduni ambako kitendo hicho kinaungwa mkono, mara nyingi hufanywa na mtabibu wa kiasili akitumia vifaa katili na bila dawa ya kuzuia maumivu.
Ukurasa kuhusu virusi vya Corona & Taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Matokeo yake ni madhara ya kiafya kimwili na kiakili kwa wanawake na wasichana. Madhara makubwa ni pamoja na kuvuja damu kupitiliza, kuhabika kwa njia ya mkojo, maumivu wakati wa tendo la ndoa na hata kuchanika kwa sehemu za njia ya mkojo na haja kubwa wakati wa kujifungua.
Dkt. Kanem anasema hata katika nchi ambako ukeketaji unapungua, bado harakati zinapaswa kuongezwa mara 10 ili kufikia lengo litakiwalo mwaka 2030. “Kufikia lengo hilo kunahitaij dola bilioni 2.4 katika kipindi cha miaka 10 ijayo, sawa na chini ya dola 100 kwa kila mtoto wa kike. Hii ni gharama ndogo sana ambayo inahitajika ili kutunza utu, afya na haki ya mtoto wa kike.”
Jukumu muhimu la wanaume na wavulana
Bi. Fore na Dkt. Kanem wamesisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano kwa mapana zaidi wakiwemo wadau mbalimbali kama vile wanaume na wavulana pamoja na mashirika ya kidini, taasisi za kusimamia sheria na haki na mahakama.
Siku ya Kimataifa
Ikiadhimishwa kila mwaka tarehe 6 mwezi Februari, siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji watoto wa kike na wanawake, inalenga kupazia sauti juhudi za kuondokana na FGM na ilitangazwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012.