Uwekezaji sahihi ni jawabu la kutokomeza FGM- Guterres

6 Februari 2022

Hoja kuu hii leo ambayo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na wasichana, au FGM, ni uwekezaji katika harakati za kutokomeza mila hiyo potofu inayotumbukiza takribani wasichana zaidi ya milioni 4 kila mwaka katika ukatili huo.

Suala hilo la uwekezaji ni ujumbe wa msingi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliotoa leo akisema cha kusikitisha zaidi janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limeathiri huduma za afya na kuwaweka wasichana na watoto wa kike katika hatari kubwa zaidi.

“Kitendo hiki dhahiri kinachoendeleza ukosefu wa usawa wa jinsia lazima kikome,” amesema Guterres akiongeza kuwa “tukiwa na uwekezaji wa dharura na wa wakati, tunaweza kufikia malengo yaliyowekwa kwenye ajenda 2030 ya maendeleo endelevu ya kutokomeza ukeketaji wa watoto wa kike ifikapo mwaka 2030 na kujenga dunia ambayo inaheshimu utu na uhuru wa mwanamke.”

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaunga mkono mipango na miradi ya kubadili imani za kijamii zinazosongesha mila hiyo potofu.

“Vijana na mashirika ya kiraia wanapaza sauti zao zisikike. Na wabunge wanasongesha wanaleta mabadiliko chanya katika nchi zao. Katika siku hii ya kutokomeza ukeketaji wa watoto wa kike na wanawake ungana nasi kutoa wito wa kulinda haki za kibinadamu za wanawake na wasichana,” ametamatisha Katibu Mkuu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter