Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaume na wavulana jitokezeni mtokomeze FGM

Msichana mwenye umri wa miaka kumi alitoroka nyumbani baada ya kugundua familia yake ilipanga kumfunza kama ngariba wa ukeketaji/C. Kwa sasa anaishi katika nyumba salama ya UNICEF huko Port Loko, Sierra Leone, na anahudhuria shule.
© UNICEF/Olivier Asselin
Msichana mwenye umri wa miaka kumi alitoroka nyumbani baada ya kugundua familia yake ilipanga kumfunza kama ngariba wa ukeketaji/C. Kwa sasa anaishi katika nyumba salama ya UNICEF huko Port Loko, Sierra Leone, na anahudhuria shule.

Wanaume na wavulana jitokezeni mtokomeze FGM

Afya

Hii leo ni ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na wasichana ,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka wanaume na wavulana wapaze sauti zao kusaidia kutokomeza mila hiyo potofu na hatarishi.  

Ujumbe wa siku hii kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia Watoto, UNICEF na lile la afya ya uzazi na idadi ya watu duniani, UNFPA ni “Nafasi ya ubia na wanaume na wavulana katika kurekebisha maadili ya kijamii na kijinsia ili kutokomeza FGM.”  

Na ndio maana katika ujumbe wake Katibu Mkuu ametanabaisha kuwa FGM imejikita katika ukosefu wa usawa kijinsia na maadili ya kijamii yanayokwamisha ushiriki wa wanawake katika uongozi, na kuwabana fursa yao ya elimu na ajira. 

Guterres amesema ubaguzi wa aina hii unaharibu jamii nzima na inahitajika hatua ya dharura ya jamii nzima kutokomeza. 

Katibu Mkuu amesema, “wanaume, wavulana kaka, baba, wahudumu wa afya, walimu na waganga wa jadi wanaweza kuwa washirika thabiti katika kuhoji na kutokomeza janga hili, kama ambavyo maudhui ya mwaka huu yanadhihirisha. Natoa wito kwa wanaume na wavulana kokote waliko waungane nami katika kupaza sauti na kujitokeza kuondoa FGM kwa maslahi ya wote.” 

Amesisitiza kuwa ukeketaji wanawake na watoto wa kike ni ukiukaji wa haki za msingi za kibinadamu unaoleta madhara ya kimwili na kiakili maisha yote ya yule aliyefanyiwa n ani moja ya vitendo vinavyosongesha mfumo dume uliojikita duniani. 

Takwimu zinaonesha kuwa takribani Watoto wa kike milioni 4.2 duniani wako hatarini kukeketwa mwaka huu wa 2023 pekee. 

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka uwekezaji wa dharura na hatua thabiti ili kufikia lengo la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs la kutokomeza kitendo hicho ifikapo mwaka 2030. 

Guterres ametamatisha ujumbe wake akitaka siku ya leo itumike kwa kila mtu kuahidi kuleta mabadiliko ya kijamii na kujenga ubia thabiti wa kutokomeza FGM sasa na wakati wote.