Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna nchi inayoweza kujikinga na majanga ya afya peke yake: Guterres

Janga la COVID-19 limerudisha nyuma miaka ya maendeleo ya kimataifa katika kukabiliana na ugonjwa wa  kifua kikuu.
© WHO/Hamad Darwish
Janga la COVID-19 limerudisha nyuma miaka ya maendeleo ya kimataifa katika kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Hakuna nchi inayoweza kujikinga na majanga ya afya peke yake: Guterres

Afya

Leo ni siku ya kimataifa ya kujiandaa na majanga afya duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku hii ametoa wito kwa nchi zote duniani kusimama pamoja na kuongeza juhudi katika kuhakikisha ulimwengu unakuwa na vifaa na upo tayari kukabiliana na changamoto za kiafya zinazokuja.

Taarifa ya ujumbe wake wa siku hii iliyotolewa hii leo jijini New York Marekani imesema miaka mitatu iliyopita mwezi kama huu dunia ilitangaziwa kuwepo wa virusi vya COVID-19, viligunduliwa na kuleta madhara makubwa duniani lakini havitakuwa vya mwisho hivyo ni vyema dunia kujiandaa.

“Janga la COVID-19 limeleta madhara kila sehemu. Mamilioni ya watu walipoteza Maisha yao, maelfu ya watu waliugua. Uchumi wa dunia uliporomoka, mifumo ya afya katika kila nchi ilizidiwa na wagonjwa na matrilioni ya dola yalipotea.” Amesema Guterres na kuongeza kuwa “Maendeleo yaliyofikiwa ya Malengo ya Maendeleo endelevu SDGs yalirudi nyuma na nchi zinazoendelea ziliachwa kujitegemea zenyewe, kwa aibu zilinyimwa chanjo, vipimo na matibabu waliyohitaji kulinda watu wao.”

WHO yatoa wito kwa nchi kuziba mapengo katika utoaji wa huduma za afya kwa watu walioathirika na migogoro na kaya zenye kipato cha chini
Natanael Melchor/Unsplash
WHO yatoa wito kwa nchi kuziba mapengo katika utoaji wa huduma za afya kwa watu walioathirika na migogoro na kaya zenye kipato cha chini

Lazima tujiandae kwa majanga mengine

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema “COVID-19 haitakuwa janga la mwisho au janga lakipekee kukabili wanadamu. Kama jumuiya ya kimataifa, ni lazima tuzingatie mafunzo makali tuliyo yaona katika janga la COVID-19 na tuwekeze kikamilifu katika kujitayarisha, kuzuia na kukabiliana na majanga ya kiafya”

Guterre amesema katika kujiandaa na majanga ya afya kunahitajika ufuatiliaji bora ili kugundua na kufuatilia virusi vilivyoko na uwezekano wa janga.

“Tunahitaji mifumo thabiti zaidi ya afya inayolenga kutoa huduma za afya kwa watu wote. Na tunahitaji wafanyakazi wa afya ambao wamefunzwa vizuri, wenye vifaa vya kutosha na wanaolipwa vizuri. Pia tunahitaji ufikiaji sawa wa chanjo, matibabu, uchunguzi na teknolojia ya kuokoa maisha kwa nchi zote.”

Katibu Mkuu Guterres pamoja na kujiandaa huko ameeleza ulazima wa kuhakikisha watu wote wanapinga habari potofuna kujikita katika taarifa sahihi zinazotolewa na zilizothibitishwa na wataalamu wa kisayansi.

Amesema pia janga linapotokea haliwezi kupigwa vita na kila nchi yenyewe badala yake linahitaji muungano wa dunia katika kupingana nalo akieleza janga la COVID-19 liilikuwa simu ya kuamsha dunia kuwa umoja ni nguvu.