UNICEF yagawa redio za sola 10,000 kusaidia watoto kusoma wakijiandaa kurejea shule Kenya 

29 Disemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF , nchini Kenya, limegawa redio 10,000 zinazotumia nishati ya sola kwa kaya masikini nchini humo ili watoto wengi wapate fursa ya kusoma nyumbani wakati huu wakijianda kurejea shuleni. 

Katika eneo la mtaa wa mabanda la Kibera jijini Nairobi, huyu ni mwanafunzi  wa sekondari Selina Nakesa Mamati anasema amekosa shule kwa miezi 8 iliyopita na yuko nyuma kimasomo endapo atarejea shuleni Januari mwakani itambidi aanze upya, na kukaa nyumbani na wazazi amechoka kwani akiamka anachokifanya ni shughuli za nyumbani na kisha ndio asome. 

Lakini sasa mambo yatabadilika kwani Selina ni miongoni mwa watoto 40,000 wanaofaidika na msaada huo wa Redio za sola baada ya UNICEF kutambua athari za kufungwa shule wakati huu wa COVID-19 hasa kwa kaya masikini. Mkuu wa mawasiliano wa shirika hilo Kenya ni Andrew Brown “Kufungwa kwa shule kumeingilia masomo kwa mamilioni ya wanafunzi nchini Kenya ambao wamekosa zaidi ya miezi sita ya masomo rasmi na wakati huo wote tumeisaidia serikali kwanza kwa watoto kusomea nyumbani na pili kwa maandalizi ya shule kufunguliwa kwa usalama” 

Kwenye maeneo duni kama Kibera sio watu wengi wanaoweza kumudu kununua redio hivyo mkurugenzi wa elimu wa kaunti Lydia Wangechi Mugeti anasema msaada wa UNICEF umekuwa ni nuru gizani kwani redio 100 zilizogawanywa katika mtaa huo wa mabanda watoto wengi zaidi wamepata fursa ya kusikiliza masomo Redioni na wale wasio nazo huenda kwa jirani wakasikiliza pia. Selina anasema  "Redio hii ya sola imemisaidia sana kwa sababu kuna vitabu ambavyo nasoma shuleni vinaitwa Kigogo, tunapokuwa shuleni tunavisoma , lakini kupitia Redio wanavisoma na pia wanatuelezea kwa kina hivyo naweza kuunda picha halisi katika fikra zangu ili niweze kuelewa vyema” 

Mama wa Selina ni Ruth Auma Mamati  kwa wanawe kusalia nyumbani bila masomo ilimuathiri pia Kutoweza kutoka nje , janga la corona sio tu kwamba liliathiri wanangu bali na mimi pia imeniathiri upande wa kazi hivyo sote tumesalia nyumbani. Imenipa changamoto nyingi sana kwa sababu wanataka kula, wanataka mahitaji ya lazima ya siku na hayo wakati mwingine hayapatikani. Unajua wakiwa shuleni inanirahisishia kazi kwa sababu wanashinda huko kuna mahitaji mengine nayaepuka” 

Ingawa ni shule chache zilizofunguliwa UNICEF inasema inaendelea kusaidia wanaosomea nyumbani hadi pale shule zote zitakapofunguliwa kwa usalama. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter