Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imetufunza mengi na hata ambayo hatukutarajia: Barubaru Termeh na Toranj 

Msichana nchini Iran akiembea karibu na mchoro wenye maandishi,"Mungu anapenda watoto wanaosema sala zao. (Maktaba).
UNICEF/Aslan Arfa
Msichana nchini Iran akiembea karibu na mchoro wenye maandishi,"Mungu anapenda watoto wanaosema sala zao. (Maktaba).

COVID-19 imetufunza mengi na hata ambayo hatukutarajia: Barubaru Termeh na Toranj 

Utamaduni na Elimu

Kutana na mapacha wawili barubaru kutoka nchini Iran, wanasema janga la corona au COVID-19 limewafunza mengi, kuanzia kusomea nyumbani, kukabiliana na upweke na msongo wa mawazo na hata kupika na  majukumu mengine ya nyumbani. 

Mapacha hawa Toranj na Termeh wenye umri wa miaka 17 wanaishi mjini Tehran nchini Iran wanasema wanaamini changamoto za shule zikimalizika maisha yatakuwa bora kwani kusoma na kufanyia mitihani nyumbani kumewapunguzia shinikizo la kuwa shuleni lakini pia kukaa nyumbani kwa muda mrefu kumewapa fursa za kujifunza mambo mengi na hata wasiyotarajia 

“Mimi ni Toranj nina umri wa miaka 17 na niko kidato cha tatu. Tunapenda kuanza siku yetu kwa kusikiliza muziki na kisha tunafanya yale yaliyopangwa kwa siku hiyo mfano kama nina kazi za shule basi naanza na hizo kwanza na kisha inabidi nimsaidie mama kusafisha nyumba na kupika na baada ya hapo ndio nafurahia kucheza.” 

Kwa Termeh hali ni tofauti ,"Mimi napenda mazingira ya nje, kitu chochote kile ili mradi kikiwa nje ninakipenda. Lakini sasa sababu ya COVID-19 tunalazimika kukaa nyumbani, na tunafanya mazoezi ili kulinda afya zetu tusiugue. Kwa maoni yangu unaweza kufanya chochote ukiwa nyumbani na pia kujifunza vitu vingi.” 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF janga la COVID-19 limewalazimisha mamilioni ya watoto kote duniani kusomea nyumbani, na wengine wanakumbana na changamoto lukuki lakini  si Termeh na Toranj kwani kwao kukaa nyumbani imekuwa faida kwao kama anavyosema Termeh “Kusema ukweli sikujua kupika chochote, sasa nimejifunza kupika vitu mbalimbali, pia nimejifunza kukabiliana na msongo wa mawazo ulioletwa na COVID-19. Tunajaribu kutowaza sana na kutumai kwamba kila kitu kitakuwa sawa hivi karibuni , lazima tuwe na matumaini kwani hali haitokuwa endelea daima.” 

Toranj anaafiki hilo na kutoa wito kwa wanafunzi wote walio majumbani kutumia fursa hiyo kujifunza vitu tofauti kwani janga la COVID-19 likiisha itakuwa ni fursa nyingine kwao ya kuanza upya wakiwa na ujuzi wa vitu mbalimbali.