UNFPA yaisaidia Ukraine kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia wakati wa COVID-19

23 Novemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA ambalo pia limejikita katika masuala ya kijinsia na afya ya uzazi limesema janga la corona au COVID-19 limekuwa ni kuongeza msumari wa moto juu ya kidonda kwa  wanawake na wasichana milioni 11 wanaopitia ukatili wa kijinsia GBV nchini Ukraine na sasa linashirikiana na programu za serikali kuzuia na kukabiliana na ukatili huo

Kwa mujibu wa shirika la UNFPA mwanamke 1 kati ya 3 nchini Ukraine amepitia ukatili uwe wa kihisia, kimwili, au kingono.  

Kristina ni miongoni mwa mamilioni ya wanawake hao na ukatili dhidi yake ulianza alipopata watoto kwani mumewe aligeuka na kuwa mgomvi na kumdhulumu kihisia.

Na baada ya miaka mingi ya kuvumilia ukatili huo Kristina aliamua kudai talaka na kuondoka kwenye nyumba yao na watoto wake. 

Lakini mumewe aliwasaka kwa udi na uvumba na kuwapata, Ksristina anasema ,Na huo ulikuwa mwanzo wa jehanamu katika maisha yetu, alinifuata kila ninakokwenda na kunitishia kama hautoishi na mimi nitajirusha dirishani”. 

Kana kwamba hiyo haitoshi anasema mumewe akamnyang’anya watoto na sasa hajawaona wanawe kwa zaidi ya mwaka mmoja. 

“Nina uchungu mkubwa moyoni nikijua kwamba wanangu hawaishi na mimi. Ninaumia sana sana.” 

Kupitia UNFPA Kristina sasa anapata msaada wa kijamii na kisheria wa kuweza kupigania haki ya kuwapata watoto wake wawili wa kiume. 

Takribani wanawake milioni 11 nchini Ukraine wamepitia aina fulani ya ukatili wa kijinsia na mamlaka ya nchi hiyo inasema mara nyingi wanawake hao hawatambui kwamba wanachopitia ni ukatili. Olena Dashutina ni afisa wa polisi  nchini humo,“Mwanzo inaonekana si kitu kikubwa lakini kadri muda unavyokwenda unaizoea tabia hiyo ambayo inaweza kuwa na athari mbaya sana , na watekelezaji wanaweza wasijue kama wanavyofanya ni vitendo vya ukatili.” 

Mwaka 2015 UNFPA kwa kushirikiana na serikali ya Ukraine walianzisha programu ya kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia ambayo hadi sasa inatoa msaada wa kijamii na kisaikolojia kwa manusura wa ukatili wa kijinsia kwa manusura kupiga simu. 

Lakini janga la COVID-19 lilipozuka mambo yakabadilika kwani ukatili umeongezeka majumbani , hata hivyo  UNFPA inasema imedhamiria kuhakikisha kwamba kwa kila njia wanawake na wasicha nchini humo wanalindwa dhidi ya ukatili huo hata wakati huu wa COVID-19. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter