Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adhabu kwa wanaofanya ukatili wa kijinsia ziongezwe

Kituo cha Maisha, waathirika wa GBV huenda hapa kusaka hifadhi kwa wakiwa na watoto wao wachanga
UN News/ Thelma Mwadzaya
Kituo cha Maisha, waathirika wa GBV huenda hapa kusaka hifadhi kwa wakiwa na watoto wao wachanga

Adhabu kwa wanaofanya ukatili wa kijinsia ziongezwe

Wanawake

Dhulma za kijinsia ni jinamizi linaloizonga jamii kote ulimwenguni.Kila mwaka, ulimwengu hutenga siku 16 za kuuelimisha umma kuhusu madhila ya dhulma za kijinsia. Kauli mbiu ya kampeni ya UniTE mwaka huu ni Tushikane: kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Kituo cha Maisha kilichoko jijini Nairobi nchini Kenya huwasitiri wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 waliobakwa au kunajisiwa. Kituo hicho kilifungua milango yake mwaka 2014 na kimefanikiwa kuwaokoa wasichana kadhaa wanaokumbana na ukatili wa kijinsia.

Usalama na amani ni haki ya wote

Kila mwanamke wa umri wowote ule ana haki ya kuwa salama na kutoandamwa na dhulma za aina yoyote. Vituo salama vya kuwahifadhi watoto waliodhulumiwa na kufanyiwa ukatili wa kijinsia ni haba jijini Nairobi na vichache vilivyoko vinabeba mzigo mzito.

Kituo cha Maisha kinawapa hifadhi wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 ambao pia wana watoto wachanga. Operesheni za kila siku zinaandamwa na changamoto za nyenzo na fedha.

Florence Keya muasisi wa kituo hicho anajua fika wanachokipitia wasichana waliodhulumiwa na kufanyiwa ukatili wa kijinsia na anaelezea mtazamo wake”Kama mtu amepitia dhulma wasilipishwe chochote mpaka wapone. Kila mara wanasema utapata matibabu ya bure lakini hilo ni kwa zile saa chache unazopewa dawa kuzuwia kupata mimba na maambukizi.”

Nilifanyiwa ukatili nikiwa mtoto

Akielezea historia ya maisha yake Florence Keya anasema yeye alidhulumiwa alipokuwa mdogo na hicho ndicho kilichomsukuma kuzindua kituo cha Maisha cha kuwapa hifadhi wasichana walionajisiwa na kubakwa.

Kulingana na tathmini ya afya na umma ya mwaka 2014 ya Kenya, 45% ya wanawake walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 wamepitia madhila ya ukatili, na 39% ya wanawake walio ndani ya ndoa wameshapitia dhulma za kijinsia au ukatili.

Naye Yvonne Njoka ambaye ni mhudumu wa jamii katika kituo cha Maisha anaelezea huduma wanazowapa wasichana waliodhulumiwa pindi wanapowapokea, “Usaidizi wa kwanza ni kumpa mavazi, malazi na chakula ili kuhakikisha ana afya njema. Baada ya ya hapo anapata ushauri nasahi na pia tunaangalia masuala ya kesi yake ama ni kortini au ofisi ya watoto kulingana na umri wake.”

Nguo za waathirika wa ukatili wa kijinsia katika kituo cha Maisha
UN News/ Thelma Mwadzaya
Nguo za waathirika wa ukatili wa kijinsia katika kituo cha Maisha

Mimba na UKIMWI

Takwimu zinaashiria kuwa Kenya ina idadi kubwa ya mimba za utotoni ambao ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 19. Katika mwaka wa 2020 na 2021 wakati janga la Corona lilipougubika ulimwengu, duru zinaeleza kuwa visa vya dhulma za kijinsia viliongezeka.

Ifahamike kuwa dhulma hizo za kijinsia aghalabu huandamana na maambukizi ya magonjwa na virusi kama vile HIV vinavyosababisha ugonjwa wa UKIMWI.

Jinamizi kubwa ni unyanyapaa katika jamii ukizingatia dhulma na HIV. Alvin Okeyo anaishi ambaye ana UKIMWI ni mshauri nasaha wa vijana na mtazamo wake unausisitizia umuhimu wa kutumia dawa ili kudhibiti hali, “Mtu akiishi na virusi vya UKIMWI hawezi kumuambukiza mwengine kama anameza dawa zake ipasavyo na kufuatilia maagizo ya daktari. Pale watu watakapoelewa kuwa unapomeza dawa na virusi vikawa havionekani unapopimwa basi huwezi kuvisambaza na hilo ndilo litakalouua unyanyapaa.”

Adhabu nyepesi kwa wanaotenda ukatili

Kulingana na shirika la matabibu wanaotetea haki za binadamu, idadi ya wanaotiwa hatiani nchini Kenya kwasababu ya kesi za dhulma za kijinsia na ukatili ni ndogo mno. Kilichochangia ni ukosefu wa ushahidi unaomhukumu mhusika mahakamani kadhalika mbinu za kuhifadhi ushahidi wa vinasaba zina mapungufu.

Yvonne Wanjiku ambaye ni mhudumu wa jamii anakiri kuwa wakati mwengine adhabau zinazotolewa na mahakama ni nyepesi kwani, “Kuna baadhi ya kesi zinachukua muda mahakamani na kisha huambulia patupu. Kesi nyingine, mhusika akihukumiwa adhabu yake inakuwa nyepesi ukizingatia ukatili aliomfanyia mtoto. Serikali inapaswa kutilia mkazo suala hilo na kubana sheria ili kuwatia hofu wahalifu.”

Florence Keya anayesimamia kituo cha kuwahifadhi watoto walionajisiwa na kubakwa anasisitiza kuwa vituo salama vya hifadhi waathirika hao vikiongezwa mambo yataimarika, “Watu wanadhulumiwa kila uchao na wanatafuta mahali pa kwenda kujisikiza kisha warejee kwenye maisha yao ya kawaida. Sio kwamba watahamia vituoni milele. Kwa mtazamo wangu tunahitaji vituo vya ziada salama vya kuwapa hifadhi wasichana na wanawake waliodhulumiwa na kufanyiwa ukatili.”

Siku 16 za elimu dhidi ya ukatili

Kila mwaka ulimwengu hushiriki kwenye kampeni ya siku 16 ya kuuelimisha umma kuhusu dhulma za kijinsia na ukatili kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Disemba. Kwa upande wake, Umoja wa mataifa ulizindua mwaka 2008 kampeni ya UniTE by 2030 inayodhamiria kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake inayofanyika sanjari na siku 16 za kuelimisha umma kuhusu dhulma za kijnsia.