Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 818 zinahitajika kutoa huduma muhimu na za kuokoa maisha kwa wanawake na wasichana walioathiriwa na mizozo-UNFPA

Manusura wa ukatili wa kijnsia ambaye anasaidiwa na misaada ya kijamii kijiji cha Bouaké, nchini Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Frank Dejongh
Manusura wa ukatili wa kijnsia ambaye anasaidiwa na misaada ya kijamii kijiji cha Bouaké, nchini Côte d'Ivoire.

Dola milioni 818 zinahitajika kutoa huduma muhimu na za kuokoa maisha kwa wanawake na wasichana walioathiriwa na mizozo-UNFPA

Haki za binadamu

Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA, leo limezindua ombi lake kubwa kuliko yote la msaada wa kibinadamu.  

Ombi hilo la dola milioni 18 za kimarekani, limetolewa hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani limesema, mwaka ujao, UNFPA inakusudia kufikia wanawake, wasichana na vijana milioni 54 katika nchi 68 kwa msaada muhimu, pamoja na huduma za afya ya uzazi na huduma za kuzuia unyanyasaji wa kijinsia na msaada kwa manusura. 

 “Janga la COVID-19 likiendelea kusumbua mifumo ya afya ulimwenguni, athari kubwa ya wanawake na wasichana katika shida za kibinadamu imezidi kuonekana. Huduma za kiafya kuhusu elimu ya yuzazi imeingiliwa, unyanyasaji wa kijinsia, GBV unazidi kuongezeka, na hitaji la msaada wa kisaikolojia linaongezeka.” Imeeleza UNFPA. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt Natalia Kanem amesema, "haki na mahitaji ya wanawake na wasichana barubaru katika dharura mara nyingi hupuuzwa, na COVID-19 imefanya mambo kuwa mabaya zaidi, na kuongezeka kwa unyanyasaji wa wenzi wa karibu, unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za utotoni. Iwe anaishi katika nyumba au hema katika kambi ya wakimbizi, kila mwanamke na msichana ana haki ya amani nyumbani. Iwe katika eneo la vita, aliyehama makazi au aliyeathiriwa na janga la asili, ana haki ya afya njema na ustawi, na kuishi kwa heshima. Ufadhili unaweza kutamka tofauti kati ya maisha na kifo katika shida. Zaidi, uwekezaji kwa wanawake na wasichana na katika uongozi wao unaboresha matarajio ya amani endelevu, ustawi na maendeleo.” 

Kupitia ombi hili la msaada wa kibinadamu, UNFPA inasisitiza hitaji la kubadilisha na kujumuisha huduma kwa afya ya kijinsia na ya uzazi, GBV na afya ya akili na msaada wa kisaikolojia wakati wa COVID-19. UNFPA pia inahitaji uwekezaji zaidi katika mashirika ya ndani yanayoongozwa na wanawake na pia mashirika ya vijana ambayo hufanya kazi kama wajibu wa mstari wa mbele. Kwa kuongezea, ombi hilo linaelezea jinsi msaada wa kibinadamu, maendeleo endelevu na ujenzi wa amani ni njia kuu za kupona kutoka kwa COVID-19. 

Katika mwaka huu wa 2020, UNFPA imefanya kazi na serikali na wadau kufikia wanawake na vijana katika maeneo yaliyokumbwa na mgogoro. Kupitia msaada huu na ushirikiano, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limewahudumia zaidi ya wanawake milioni 7 katika nchi 53 kuhusu huduma kijinsia na afya ya uzazi, watu milioni 4.4 katika nchi 49 katika masuala ya mpango wa uzazi na watu milioni 2.8 katika huduma za kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia.