Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pikipiki za magurudumu matatu na mashua kutumika kusambaza chakula na pesa Nigeria

WFP inasambaza vyakula kwakutumia pikipiki za magurudumu matatu maarufu Kéké katika mji wa Kano, Nigeria.
WFP/Photogallery
WFP inasambaza vyakula kwakutumia pikipiki za magurudumu matatu maarufu Kéké katika mji wa Kano, Nigeria.

Pikipiki za magurudumu matatu na mashua kutumika kusambaza chakula na pesa Nigeria

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP na serikali ya Nigeria wamezindua programu ya msaada wa chakula na fedha taslimu katika maeneo matatu ya mijini yaani Abuja, Kano na Lagos ambako kote huko ni kitovu cha COVID-19 nchini humo. 

Taarifa ya shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP iliyotolewa mjini Kano Nigeria imeeleza kuwa shirika hilo limeamua kutoa dola za kimarekani milioni 3 ili kutoa msaada wa fedha taslimu kwa watu walioathirika zaidi na COVID-19 nchini Nigeria na kuongeza nguvu katika juhudi za serikali ya nchi hiyo ambayo imetoa tani 2,000 za chakula kutoka katika hifadhi yake ya kimkakati ya nafaka, kiasi ambacho kina thamani ya dola milioni 1 za kimarekani.  

Ikishirikiana na wizara ya serikali kuu ya shirikisho inayohusika na masuala ya kibinadamu, usimamizi wa maafa na maendeleo ya jamii, hii ni mara ya kwanza ambapo WFP inapanua mpango wake nchini Nigeria ili kuwafikia watu katika miji na majiji ambako mamilioni ya watu wanatishiwa na njaa na utapiamlo kutokana na anguko la kijamii na kiuchumi kwasababu ya janga la COVID-19. 

Kote nchini Nigeria, nchi yenye uchumi wa juu na pia yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, watu ambao wana kipato kidogo wamepoteza zaidi ikiwa ni matokeo ya janga la virusi vya corona. Taarifa ya WFP inaeleza kuwa takribani asilimia 90 ya watu wanategemea kipato cha kila siku na wengi wa watu hawa wanaishi katika maeneo ya mijini na kwamba wafanyakazi hawa wa kazi zisizo rasmi  wamepoteza hadi asilimia 80 ya kipato chao. “Bei ya vyakula imepanda na ili waweze kuendana na hali, familia zimelazimika kukopa fedha na chakula, au kuuza mali zao zilizokuwa zimesalia na hivyo kuzama zaidi katika lindi la umaskini.” Imesisitiza WFP. 

Katika Mkutano wa pamoja wa WFP na Nigeria kwa waaandishi wa habari, Gavana Abdullah Umar Ganduje wa jimbo la Kano amesema, “ushirikiano huu umetuwezesha kuokoa maisha ya maelfu ya watu katika jimbo la Kano katika nyakati hizi ngumu.” 

Usambazaji wa pesa na chakula umeanza katika Jimbo la Kano ili kusaidia juhudi zinazoendelea za Serikali za kukomesha athari za janga hilo. Katika wiki na miezi ijayo, WFP itaendelea kufanya kazi na Serikali za Abuja na Lagos kusaidia familia zilizo hatarini zaidi. 

Ili kupunguza hatari ya kuambukizwa virusi, WFP imepanga kupeleka nyumbani pesa taslim na chakula. Katika jimbo la Kano chakula kitapelekwa kwa kutumia huduma ya pikipiki za magurudumu matatu maarufu Kéké. Jijini Lagos, WFP inashirikiana na Serikali ya Jimbo kupeleka chakula kwa kutumia mashua kuzifikia familia zinazoishi katika mwambao wa eneo la Makoko. Wakati huo huo, katika maeneo yote ya mijini, pesa zitahamishwa kupitia kadi za malipo au uhamisho wa benki mtandaoni. 

 “Serikali ya Nigeria imeonesha kujitolea na uongozi mkubwa katika kushughulikia janga hili. Hili ndilo hasa tunalohitaji wakati huu wa janga na zaidi kufikia kutokomeza njaa nchini Nigeria.” Amesema Paul Howe, Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP nchini Nigeria.