Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia za raia wa Nigeria ambao tayari wameathiriwa na migogoro, na sasa COVID-19, ‘wako mahututi’

Watoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani iliyoko Maiduguri, Borno, Nigeria
IOM/Jorge Galindo
Watoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani iliyoko Maiduguri, Borno, Nigeria

Familia za raia wa Nigeria ambao tayari wameathiriwa na migogoro, na sasa COVID-19, ‘wako mahututi’

Msaada wa Kibinadamu

Msaada na ufadhili vinahitajika haraka kwa mamilioni ya watu nchini Nigeria kwa watu ambao wamepigwa vikali na madhara ya mlipuko wa virusi vya corona au COVID-19 zikiwemo jamii zinazotegemea misaada kuishi kaskazini mashariki mwa nchi kutokana na migogoro, imesema hii leo ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya dharura, OCHA.

Nalo shirika la chakula duniani WFP limesema kiasi cha fedha zaidi ya dola milioni 182 zinahitajika katika miezi sita ijayo ili kuendeleza misaada ya uokoaji wa maisha kwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.

Msemaji Mkuu wa WFP Elisabeth Byrs, akizungumzia kuhusu maeneo ya Borno, Adamawa na Yobe amesema, “tuna wasiwasi na jamii zilizoathiriwa na migogoro kaskazini mashariki mwa Nigeria ambao tayari wanakabiliwa na njaa kali na ambao wako hatarini. Wako katika hali ya umaututi na wanahitaji msaada kuweza kuishi.”

 Majimbo hayo matatu yanayofahamika nchini Nigeria kwa kifupi kama BAY yamekuwa katika mgogoro mkubwa wa muda mrefu ambao umesambaa kote katika ukanda wa ziwa Chad.

Virusi vya corona

Kufikia hivi sasa, takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa Nigeria imekuwa na wagonjwa 12,800 wa ugonjwa wa COVID-19 na vifo 360 vimetokea vikihusishwa na ugonjwa wa upumuaji.

Zaidi ya watu milioni 3.8 hususani wanaofanya kazi katika sekta binafsi wanakabiliwa na kupoteza kazi kutokana na kuongezeka kwa ugumu wa maisha, amesema Bi Byrs na kuwa hali hiyo inaweza kuongezeka kufikia watu milioni 13 ikiwa vikwazo vya kutembea kutoka eneo moja kwenda jingine vitaendelea kwa muda mrefu.

“Hii itaongeza katika takribani watu milioni 20 ambao ni asilimia 23 ya nguvu kazi ambao tayari wako nje ya kazi.” Ameeleza msemaji huyo wa WFP.