Heko serikali zilizochukua hatua za kijasiri na kuwezesha watoto kurejea shuleni - UNICEF
Heko serikali zilizochukua hatua za kijasiri na kuwezesha watoto kurejea shuleni - UNICEF
Ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ulipovuruga mwenendo wa elimu duniani, kila mtu alisalia na maswali mengi! Je tufanye vipi watoto waweze kuendelea kujifunza? Tufanye vipi ili kuhakikisha watoto wanapata msaada muhimu kupitia shule ikiwemo mlo wenye lishe?
Hayo ni maswali ambayo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na wadau walijiuliza kuanzia mwezi Machi mwaka huu COVID-19 ilipotangazwa kuwa janga la kimataifa.
Maswali yaliendelea, mfano! Kwa vipi shule zitafunguliwa tena huku usalama wa watoto ukipatiwa kipaumbele?
Lakini baada ya muda, mambo mengi yamefahamika na UNICEF na wadau wake wamejifunza mambo mengi na kile cha kufanya.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore anataja mambo makuu manne ambayo serikali zinapaswa kuzingatia.
Mosi ni kutochangamana pamoja na usafi.
Ametoa mfano wa “nchini Senegal, shule zimehakikisha kuna kutochangamana miongoni mwa watoto kwa kuongeza nafasi kati ya mwanafunzi na mwanafunzi darasani. Serikali kuanzia Afghanistan hadi Albania zimeimarisha huduma za kunawa mikono na usafi shuleni na zimeweka kanuni za uchunguzi wa afya. Shule nyingi zimeachana na michezo ya ndani na sasa watoto wanacheza nje.”
Halikadhalika amesema shule zinahamasisha unawaji mikono ili kusaidia watoto wawe salama iwe shuleni au nyumbani.
Hatua ya pili ni ufundishaji unaoendana na hali halisi
Bi. Fore amesema, “nchi kama Misri, Namibia na Papua New Guinea zimeanzisha madarasa madogo na zimeongeza muda wa masomo ili kuhakikisha watoto wanasoma kwa zamu. Rwanda inajenga madarasa mapya na kuajiri walimu zaidi ili kuepusha msongamano darasani. Italia inaajiri walimu wa muda mfupi ili kusaidia kufundisha.”
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF amesema nchini nyingi zinatumia ufundishaji mchanganyiko ikimaanisha kwamba, “watoto wanafundishwa darasani na vile vile wakiwa nyumbani.”
Nchi zingine zimeondoa walimu kutoka katika majukumu ya hatari zaidi hadi majukumu yenye hatari kidogo.
Hatua ya tatu ni ufunguaij wa shule kwa awamu
Mataifa kama vile China, Indonesia na Uruguay yanachukua hatua kwa hatua katika ufunguaji wa shule zao.
“Mathalani, wanaweza kuanza na maeneo yenye hatari kidogo zaidi ya kupata COVID-19 au wakaanza na wanafunzi wadogo kwanza. Hii inatoa fursa ya kufanyia majaribio kanuni za usalama na kujumuisha wazazi, walimu na wanafunzi,” amesema Bi. Fore.
Hatua ya nne ni jinsi ya kufikia watoto walio hatarini zaidi
UNICEF inashirikiana na serikali ya Burkina Faso kuhamasisha kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike wakati huu wa kampeni za kurejea tena shuleni.
“Inatia moyo sana kuona wanafunzi, wazazi, walimu na watunga sera wakichukua hatua za kukabili janga hili. Tunatiwa moyo pia na nchi kama Burundi, Uholanzi na Denmark. Hizi zimefungua shule bila kushuhudia ongezeko la maambukizi ya COVID-19, au ongezeko la kusambaa kwa virusi miongoni mwa wanajamii,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF.
Ukurasa kuhusu Virusi vya Corona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Amesema kwa upande wao, Israel, Ufaransa na China, zilidhibiti haraka sana mlipuko wa Corona kwenye baadhi ya maeneo pindi tu taarifa zilipopatikana.
Ni kwa mantiki hiyo amesema kuwa UNICEF inaendelea kutoa wito kwa serikali kupatia kipaumbele suala la ufunguaji wa shule na zichukue hatua mujarabu kudhibiti maambukizi.
Amekumbusha kuwa kitendo cha shule kufungwa, kimekuwa na madhara mabaya sana kwa watoto ambapo watoto walio pembezoni ndio wameathirika zaidi.
“Sasa ni wakati wa kusaidia na kuwekezaji haraka kwenye elimu kwa kila mtoto,” ametamatisha Bi. Fore.