Skip to main content

UNICEF yahimiza serikali duniani kufungua shule, japo kwa tahadhari

Msichana kutoka Kenya akisomea nyumbani wakati wa vikwazo kukabiliana na janga la COVID-19.
© UNICEF/Brian Otieno
Msichana kutoka Kenya akisomea nyumbani wakati wa vikwazo kukabiliana na janga la COVID-19.

UNICEF yahimiza serikali duniani kufungua shule, japo kwa tahadhari

Utamaduni na Elimu

Idadi ya watoto wa shule walioathiriwa na kufungwa kwa shule kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 imeongezeka kwa asilimia 38 mwezi uliopita wa  Novemba, hali hiyo ikiweka mkwamo mkubwa kwenye maendeleo ya masomo na ustawi wa wanafunzi zaidi ya milioni 90 ulimwenguni, limeeleza shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa hii leo mjini New York imeeleza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na UNESCO, vyumba vya madarasa kwa takribani mtoto 1 kati ya watoto wa shule 5 ulimwenguni au sawa na watoto milioni 320, hadi kufikia tarehe mosi ya mwezi huu wa Desemba,  yamefungwa, ambalo ni ongezeko la karibu milioni 90 kutoka milioni 232 mnamo Novemba mosi. Kwa upande mwingine, mwezi wa Oktoba idadi ya watoto wa shule walioathiriwa na kufungwa kwa shule ilipungua karibu mara tatu. 

UNICEF imeeleza kuwa wakati shule zinapofungwa, watoto huwa hatarini kupoteza masomo yao, mfumo wa msaada, chakula na usalama, na watoto walio katika hali duni zaidi ambao wana uwezekano mkubwa wa kuacha kabisa shule, wakiathirika zaidi. Na, wakati mamilioni ya watoto wanabaki nje ya vyumba vyao vya madarasa kwa zaidi ya miezi tisa, na wengi zaidi wanaishi tena katika machafuko, UNICEF inaogopa kwamba shule nyingi zinafungwa bila ya ulazima, na hakuna mkazo wa kutosha uliowekwa katika kuchukua hatua zinazohitajika kufanya shule ziwe mahali salama dhidi ya COVID-19

Utafiti wa hivi karibuni unaotumia data kutoka nchi 191 haukuonesha uhusiano wowote kati ya hali ya shule na viwango vya maambukizi ya COVID-19 katika jamii. Ukiwa na ushahidi mdogo kwamba shule zinachangia viwango vya juu vya maambukizi, UNICEF inahimiza serikali kuweka kipaumbele kufungua shule na kuchukua hatua zote zinazowezekana kuzifanya kuwa salama kadri inavyowezekana. 

Mkuu wa elimu wa UNICEF, Robert Jenkins amesema, “ushahidi unaonesha kuwa shule sio sababu kuu za janga hili. Japo tunaona mwenendo wa kutisha ambapo serikali zinafunga shule tena kama njia ya kwanza badala ya suluhisho la mwisho. Katika maeneo mengine, hii inafanywa nchi nzima, badala ya jamii kwa jamii, na watoto wanaendelea kupata athari mbaya kwa ujifunzaji wao, ustawi wa akili na mwili na usalama. " 

Mipango ya kufungua shule lazima ijumuishe kupanua upatikanaji wa elimu, pamoja na ujifunzaji nje ya shule, hasa kwa vikundi vilivyombali katika hali duni. Mifumo ya elimu pia inapaswa kubadilishwa na kujengwa kuhimili majanga ya baadaye, UNICEF imeshauri. 

Mfumo wa UNICEF wa kufungua shule, uliotolewa kwa pamoja na UNESCO, UNHCR, WFP na Benki ya Dunia, unatoa ushauri wa vitendo kwa mamlaka ya kitaifa na ya mitaa. Miongozo hiyo inazingatia mageuzi ya sera, mahitaji ya fedha, shughuli salama, afya na ulinzi na kufikia watoto waliotengwa zaidi.