Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Timu ya WHO ya kupambana na polio Pakistan yasaidia vita dhidi ya COVID-19

Muhudumu wa afya akimpa chanjo ya polio binti wa miaka 4 nyumbani kwao Bhatti Gate mjini Lahore jimbo la Punjab nchini Pakistan
UNICEF/Asad Zaidi
Muhudumu wa afya akimpa chanjo ya polio binti wa miaka 4 nyumbani kwao Bhatti Gate mjini Lahore jimbo la Punjab nchini Pakistan

Timu ya WHO ya kupambana na polio Pakistan yasaidia vita dhidi ya COVID-19

Afya

 Timu ya shirika la afya duniani WHO inayohusika na kutokomeza polio imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kusaidia hatua za kupambana na janga la corona au COVID-19 kwa kushirikiana na serikali ya Pakistan tangu mwanzo wa mlipuko wa ugonjwa huo huku ikiendelea na kazi ya kutokomeza polio. 

Mjini Peshawar nchini Pakistan pilikapilika za kila siku zikiendelea mitaani , lakini ni dhahiri mji huu ambao unakabiliwa na tatizo kubwa la polio corona pia inaleta changamoto kubwa. 

Na sasa msaada mkubwa unatolewa kutoka kwenye programu ya serikali ya Pakistan na WHO ya kutokomeza polio ili kusaidia kupambana na mlipuko huo japo katika hospitali za mji huu suala la polio bado linapewa kipuaumbele kikubwa pia. 

Na ofisi za WHO mjini Islamabad zinashirikiana kwa karibu na serikali ya Pakistan kukabili majanga haya yote mawili. 

Mwakilishi wa WHO Pakistan ni Dkt.Palitha Mahipala anasema hatua za serikali ya Pakistan kupambana na COVID-19 ni kubwa na za kina na kwamba miundombinu iliyowekwa kwa ajili ya polio imekuwa mkombozi wa vita dhidi ya COVID-19

“Na pia wahudumu wa afya wa polio walihusika katika kutoa mafunzo ya haraka kwa timu na wahudumu wa afya walio msitari wa mbele kukabili janga hili katika utekelezaji wa kuzuia maambukizi na kudhibiti na kisha kujihusisha na tathimini ya vituo vya kuarantini. Hivyo mchango wa wahudumu wa polio ni mkubwa sana na huo ni mfano mzuri kwa nchi nyingine. "

Nchini Afghanistan, baba akisaidia kakimbembeleza mtoto wake wakati muhudumu wa afya akimpatia chanjo ya polio.
UNICEF
Nchini Afghanistan, baba akisaidia kakimbembeleza mtoto wake wakati muhudumu wa afya akimpatia chanjo ya polio.

Mjini Peshawar WHO inasema miongoni mwa mbinu zilizosaidia sana kufuatilia na kupambana na ugonjwa wa polio zimetumika sasa kama mfano bora kwa COVID-19 ikiwemo kutumia mitandao maalum iliyoweka katika hospitali na vituo vya afya, lakini pia kila wakati kukusanya na kupima maji 

Na mifumo ya takwimu iliyoko nchi nzima vikiwemo vituo vya kupiga na kupokea simu mjini Islamabad vimesaidia kukabiliana na taarifa potofu na kubaini wagonjwa. 

Kituo cha kitaifa cha dharura cha kupokea simu cha Sehat Tahaffuz 1166 kimezidi kuwa jukwaa muhimu la kusikiza malalamiko ya watu na kuwapa taarifa sahihi Dkt. Afifa Younas Raja ni daktarin katika kituo hicho 

“Jukumu lilikuwa na changamoto kubwa hasa ukizingatia hivi ni vurus vipya na taarifa kuhusu virus hivi zilikuwa haba tulipoanza, lakini tunashukuru kwa msaada wa WHO tumepata mwongozo wa kufuata na imetusaidia sana kujiandaa.” 

Awali kituo hicho kilikuwa kinapokea mamia ya simu kwa siku lakini tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 idadi iliongezeka na kufikia simu 50,000 kwa siku hasa wakati wa Juni na Julai janga hilo liliposhika kasi.