Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya juu ya hatari ya mlipuko wa magonjwa huku mafuriko yakiendelea Pakistan

Tangu katikati ya Juni mafuriko na maporomoko ya udongo yameiathiri Pakistan kufuatia mvua kubwa za Monsoon zilizosababisha uharibifu mkubwa
© WFP/Saiyna Bashir
Tangu katikati ya Juni mafuriko na maporomoko ya udongo yameiathiri Pakistan kufuatia mvua kubwa za Monsoon zilizosababisha uharibifu mkubwa

WHO yaonya juu ya hatari ya mlipuko wa magonjwa huku mafuriko yakiendelea Pakistan

Afya

Hatari kubwa za kiafya zinajitokeza nchini Pakistan huku mafuriko ambayo hayajawahi kushuhudiwa yakiendelea, limeonya leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa ulimwenguni (WHO)na kuongeza kuwa kuna hatari ya kuzuka na kuenea kwa magonjwa ya malaria, homa ya kidingapopo na magonjwa mengine yanayoenezwa na maji na wadudu.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limeainisha hali hiyo kama hali ya dharura ya daraja la 3  ambacho ni kiwango cha juu zaidi cha mfumo wake wa uwekaji alama za ndani  na hii inamaana kwamba ngazi zote tatu za shirika hilo zinahusika katika hatua za kukabili hali hiyo zikiwemo za nchi na ofisi za kikanda, pia ikiwemo makao yake makuu mjini Geneva.

Akitoa taarifa kutoka makao makuu ya WHO Dkt. Tedross amesema "Mafuriko nchini Pakistan, ukame na njaa katika Pembe kubwa ya Afrika, na vimbunga vikali vya mara kwa mara katika ukanda wa Pasifiki na Karibbea vyote vinaashiria hitaji la haraka la kuchukua hatua dhidi ya tishio lililopo la mabadiliko ya tabianchi.”

Mamilioni ya watu wameathirika

Zaidi ya watu milioni 33 nchini Pakistani, na robo tatu ya wilaya zote, wameathiriwa na mafuriko hayo yaliyoletwa na mvua za masika zijulikanazo kama Monsoon.

Mvua kubwa na mafuriko vimewalazimisha maelfu ya watu kutoka kwenye nyumba zao Balochistan
© UNICEF/Abdul Sami Malik
Mvua kubwa na mafuriko vimewalazimisha maelfu ya watu kutoka kwenye nyumba zao Balochistan

Takriban watu 1,000 wamepoteza maisha na 1,500 kujeruhiwa, limesema shirika la WHO likinukuu mamlaka ya afya ya kitaifa na kuongeza kuwa watu wengine zaidi ya 161,000 sasa wanapata hifadhi makambini.

Takriban vituo 900 vya afya kote nchini vimeharibika, ambapo 180 kati ya hivyo vimesambaratika kabisa na kuwaacha mamilioni ya watu bila kupata huduma za afya na matibabu.

Serikali ya Pakistan imetangaza hali ya hatari, na Umoja wa Mataifa umezindua ombi la dola milioni 160 kwa nchi hiyo. 

Tedros pia ametoa dola milioni 10 kutoka kwa mfuko wa dharura wa WHO kusaidia hatua za msaada.

Kutoa vifaa vya kuokoa maisha

"WHO imeanzisha hatua za haraka za kutibu majeruhi, kutoa vifaa vya kuokoa maisha kwa vituo vya afya, kusaidia timu za afya zinazohamishika, na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza," amesema Dkt. Ahmed Al-Mandhari, mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Mediterania.

WHO na washirika wake wamefanya tathmini ya awali ambayo imefichua kwamba kiwango cha sasa cha uharibifu ni kikubwa zaidi kuliko mafuriko ya awali, ikiwa ni pamoja na yale yaliyoharibu karibu nchi nzima mwaka 2010.

Watoto walioathirika na mafuriko nchini Pakistan wakipimwa na wataalam wa afya
© UNICEF/UN0691115/Sami Malik
Watoto walioathirika na mafuriko nchini Pakistan wakipimwa na wataalam wa afya

Kuhakikisha upatikanaji wa huduma

Mgogoro huo umezidisha milipuko ya magonjwa, ikijumuisha kuhara kwa sababu ya maji, homa ya kidingapopo, malaria, polio, na COVID-19, haswa katika kambi na ambapo vifaa vya maji na vyoo vimeharibiwa.

Pakistan tayari ilikuwa imerekodi visa 4,531 vya surua mwaka huu, na visa 15 vya virusi vya polio mwitu, hata kabla ya mvua kubwa na mafuriko. 

Hivi sasa kampeni ya kitaifa ya polio imetatizwa katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

"WHO inafanya kazi na mamlaka ya afya kuchukua hatua haraka na kwa ufanisi mashinani. Vipaumbele vyetu muhimu sasa ni kuhakikisha upatikanaji wa haraka wa huduma muhimu za afya kwa watu walioathiriwa na mafuriko kuimarisha na kupanua ufuatiliaji wa magonjwa, kuzuia na kudhibiti milipuko, na kuhakikisha uratibu thabiti wa nguzo za afya," amesema Dkt. Palitha Mahipala, Mwakilishi wa WHO nchini Pakistan.