Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msumbiji imethibitisha kuzuka kisa kipya cha polio:WHO

Muuguzi akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto mchanga katika hospitali nchini Malawi
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Muuguzi akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto mchanga katika hospitali nchini Malawi

Msumbiji imethibitisha kuzuka kisa kipya cha polio:WHO

Afya

Mamlaka ya afya nchini Msumbiji leo imetangaza mlipuko wa virusi vya polio aina ya 1 baada ya kuthibitisha kwamba mtoto katika jimbo la kaskazini-mashariki la Tete nchini humo aliambukizwa ugonjwa huo kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO. 

Shirika hilo limesema hiki ni kisa cha pili kilichoingizwa kutoka nje cha virusi vya polio kusini mwa Afrika mwaka huu, kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo nchini Malawi katikati ya mwezi wa Februari. 

 Hadi sasa, kuna kisa kimoja tu nchini Msumbiji na cha kwanza kugunduliwa nchini humo tangu mwaka 1992.  

WHO inasema virusi hivyo vimebainika  kwa mtoto ambaye alianza kupata ugonjwa wa kupooza mwishoni mwa mwezi Machi.  

Uchanganuzi wa mpangilio wa jenasi unaonyesha kuwa kisa kipya kilichothibitishwa kinahusishwa na aina ya polio ambayo ilikuwa ikisambaa nchini Pakistan mwaka 2019, sawa na kesi iliyoripotiwa nchini Malawi mapema mwaka huu. 

Kisa hicho akiathiri utokomezwaji wa polio Afrika 

Kwa mujibu wa WHO kisa hiki kipya nchini Msumbiji na kile ya awali nchini Malawi haviathiri uidhinishaji au utokomezwaji wa virusi vya polio barani Afrika kwa sababu aina ya virusi hivyo si ya kiasili.  

Afrika ilitangazwa kuwa haina tena virusi pori vya polio Agosti 2020 baada ya kuondoa aina zote za polio mwitu katika ukanda hilo. 

 "Kugunduliwa kwa kisa kingine cha virusi vya polio mwitu barani Afrika kunatia wasiwasi sana, hata kama haishangazi kutokana na mlipuko wa hivi karibuni  nchini Malawi. Hata hivyo, inaonyesha jinsi virusi hivi vilivyo hatari na jinsi vinavyoweza kuenea kwa haraka,” amesema Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa shirika la afya ulimwenguni kanda ya Afrika.  

Ameongeza kuwa "Tunaunga mkono serikali za kusini mwa Afrika kuongeza mapambano dhidi ya polio ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni kubwa za chanjo zinazofaa kukomesha virusi na kuwalinda watoto kutokana na athari zake mbaya." 

 Uchunguzi zaidi unaendelea nchini Msumbiji ili kubaini ukubwa wa hatari inayoletwa na kisa kipya cha virusi vya polio na hatua zinazohitajika.  

Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio
WHO
Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio

Uchambuzi wa awali wa sampuli zilizokusanywa kutoka kwa watu watatu walio karibu na kisa kipya kilichogunduliwa zote zilikuwa hasi kwa virusi vya polio aina ya 1. 

Kampeni ya polio 

 Msumbiji hivi karibuni kumefanya kampeni mbili kubwa za chanjo katika kukabiliana na mlipuko wa Malawi ambapo watoto milioni 4.2 walichanjwa dhidi ya ugonjwa huo.  

WHO inasema juhudi kwa sasa zinaendelea kusaidia kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika nchi za Malawi, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.  

Nchi hizo tano zitaendelea na chanjo hiyo kwa wingi, huku kukiwa na mipango ya kuwafikia watoto milioni 23 wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa chanjo ya polio katika wiki zijazo. 

 Duniani kote, virusi vya polio mwitu hupatikana tu nchini Afghanistan na Pakistan. Polio inaambukiza sana na huathiri sana watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.  

Hakuna tiba ya polio, na inaweza tu kuzuiwa kwa chanjo. Watoto kote ulimwenguni wanasalia katika hatari ya kupata polio aina ya 1 endapo virusi hivyo havijatokomezwa katika maeneo yaliyosalia ambayo bado vinasambaa.