Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF kuongoza mchakato wa upatikanaji na usamabazaji wa chanjo za COVID-19 

Wafanyakazi wa UNICEF wakipakua dawa katika hospitali moja magharibi mwa Venezuela.
© UNICEF/Montico
Wafanyakazi wa UNICEF wakipakua dawa katika hospitali moja magharibi mwa Venezuela.

UNICEF kuongoza mchakato wa upatikanaji na usamabazaji wa chanjo za COVID-19 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF litafanya kazi kwa karibu na makumpuni wazalishaji wa madawa na washirika wengine katika uhakikisha upatikanaji wa dozi za chanjo ya Corona au COVID-19, usafirishaji, na uhifadhi wake kwa niaba ya kituo cha kimataifa cha COVAX. 

UNICEF inaongoza juhudi hizo za upatikanaji na usambazaji wa chanjo ya COVID-19 katika kile kinachowezekana kuwa operesheni kubwa zaidi duniani na ya haraka ya upatikanaji na usambazaji wa chanjo kama sehemu ya mpango wa kimataifa wa chanjo wa COVAX unaosimwamiwa na muungano wa chanjo duniani Gavi. 

Wakati aina mbalimbali za chanjo zikionyesha matumaini, UNICEF kwa kushirikiana na shirika la afya kwa nchi za Amerika PAHO wataongoza juhudi hizo ili kupata chanjo kwa ajili ya nchi 92 za kipato cha chini na zile zinazoelekea kipato cha wastani ambazo ununuzi wa chanjo zake utapigwa jeki na mkakati maalum wa Gavi COVAX. 

Lakini pia UNICEF itakuwa ndio mratibu wa upatikanaji wa chanjo hiyo pia kwa ajili ya nchi 80 za kipato cha juu ambazo zimeonyesha dhamira ya kushiriki mchakato wa COVAX na zitagharamia chanjo hizo kwa kutumia bajeti zao binafsi. 

Wengine watakaoshirikiana na UNICEF kufanikisha hilo ni shirika la afya duniani WHO, muungano wa chanjo GAVI, CEPI, PAHO, Benki ya Dunia, wakfu wa Bill na Melinda gates na wadau wengine. 

Kituo cha COAX kiko wazi kwa ajili ya nchi zote ili kuhakikisha hakuna nchi itakayosalia nyuma bila kupata fursa ya chanjo ya COVID-19 itaapopatikana.

Kuhusu jukumu hilo kubwa la UNICEF mkurugenzi mtendaji wake Henrietta Fore amesema “Huu ni ushirika wa nguvu baina ya serikali, makampuni ya utengenezaji wa dawa na wadau wengine balimbali wa kuendeleza vita dhidi ya janga la COVID-19. Katika nia yetu ya pamoja ya kusaka chanjo, UNICEF inatumia uwezo wake wa kipekee katika usambazaji wa chanjo kuhakikisha kwamba nchi zote zina fursa salama , ya haraka na iliyo sawa katika kupata chanjo za awali punde zitakapopatikana.” 

UNICEF ndio mnunuzi mubwa zaidi wa chanjo duniani ambapo kila mwaka hununua zaidi ya dozi bilioni 2 za chanjo kwa ajili ya kampeni za kawaida za chanjo na kukabiliana na milipuko ya magonjwa mbalimbali kwa niaba ya karibu nchi 100 duniani. 

Lakini pia ni mdau mkubwa wa GAVI ambapo kwa zaidi ya miaka 20 UNICEF imeweza kuwafikia zaidi ya watoto milioni 760 na chanjo za kuokoa maisha na hivyo kuzuia zaidi ya vifo milioni 13. 

UNICEF itatumia utaalm wake kuhusu usakaji na masoko kuratibu upatikanaji na usambazaji wa chanjo za COVID-19 kwa ajili ya kituo cha COVAX.