Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa janga la COVID-19 kuna nuru gizani:Guterres

UNICEF ikifikisha shehena ya chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Msumbiji
UNICEF
UNICEF ikifikisha shehena ya chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Msumbiji

Mwaka mmoja wa janga la COVID-19 kuna nuru gizani:Guterres

Afya

Baada ya miezi 12 ya ulimwengu kukabiliwa na "tsunami ya mateso", kuwasili kwa chanjo dhidi ya janga la corona au COVID-19 inashiria nuru fulani baada ya kiza totoro" amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo Alhamisi,ikiwa ni maadhimisho yam waka mmoja tangu shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO) ) kutangaza rasmi kuwa janga hilo ni la kimataifa.

"Maisha ya watu wengi yamepotea, huku uchumi ukisimama na jamii zikiachwa kutetereka. Walio hatarini zaidi wameteseka zaidi. Waliobaki nyuma wanaachwa nyuma zaidi. " ameongeza Antonio Guterres katika ujumbe wake.

Pia amepongeza juhudi zinazofanyika kote duniani za kubadilika, na kuishi kwa njia ya habari, kuwaenzi wahudumu wa sekta ya afya "kwa kujitolea kwao na jitihada na wafanyikazi wengine wote muhimu ambao wamefanya jamii ziendelee na maisha. Ninawaheshimu wale wote ambao wamesimama kidete kupinga wapotoshaji na Habari za uongo, na ambao wamefuata itifaki za kisayansi na usalama, mmesaidia kuokoa maisha."

Muhimu ni chanjo kwa wote

Guterres amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuhamasisha jamii ya kimataifa kutekeleza ahadi ya mpango wa chanjo sawa kwa wote wa COVAX, na kuzifanya "ziwe za bei rahisi na zinazopatikana kwa wote, na kwa bei nafuu zaidi, na pia kuweka kipaumbele maalum kwa mahitaji ya wale ambao wamebeba mzigo wa janga hili kwa kiwango kikubwa  hasa wanawake, makundi ya walio wachache, wazee, watu wenye ulemavu, wakimbizi, wahamiaji na watu wa asili."

Ushirikiano wa kimataifa kupitia mkakati wa COVAX  umewezesha chanjo kufika SUDAN na pichani mhudumu wa afya akionesha alama ya ushindi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya CORONA.
© UNICEF/Ahmed Salim Yeslam
Ushirikiano wa kimataifa kupitia mkakati wa COVAX umewezesha chanjo kufika SUDAN na pichani mhudumu wa afya akionesha alama ya ushindi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya CORONA.

Kwa jumla, pamoja na juhudi za maendeleo ya kasi ya upatikanaji wa chanjo katika nchi nyingi ulimwenguni, "kuna nuru baada ya kughubikwa na giza nene" amesema Katibu Mkuu huku akiusifu kuanza kwa utoaji wa kihistoria wa chanjo wiki iliyopita kupitia mkakati wa chanko wa COVAX, uliosaidia kufikisha chanjo kwa mataifa yenye kipato cha chini duniani.”

"Walakini nina wasiwasi sana kwamba nchi nyingi za kipato cha chini bado hazijapata hata dozi moja ya chanjo, wakati nchi tajiri ziko njiani kuchanja watu wao wote", ameongeza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, akiangazia kile alichosema ni mifano mingi ya "utaifa au ubinafsi wa chanjo na kujilimbikizia chanjo katika mataifa tajiri yanayofanyika, pamoja na mikataba yakando inayohusisha watengenezaji.

‘Mtihani mkubwa wa maadili’

Bwana Guterres amesema "Kampeni ya chanjo duniani inawakilisha mtihani mkubwa zaidi wa kimaadili katika zama zetu.”

Ni muhimu pia kufufua upya uchumi wa dunia na kusaidia ulimwengu kuondoka kutoka kuzifunga jamii hadi kutokomeza virusi. Chanjo za COVID-19 lazima zionekane kama ni faida ya umma ulimwenguni. 

Dunia inahitaji kushikamana ili kuzalisha na kusambaza chanjo za kutosha kwa wote, ambazo zinamaanisha angalau kuongeza uwezo wa utengenezaji mara dufu kote duniani. Ameendelea Guterres.

“Jitihada hizo lazima zianze sasa. Ni pamoja tu tunaweza kumaliza janga hili na kujikwamua. ”

Bwana Guterres amesisitiza kwamba mshikamano ndio ufunguo, na kuundwa kwa umoja wa kweli. "Ni pamoja tu tunaweza kufufua uchumi wetu. Na kisha, pamoja, tunaweza kurudi kwenye vitu tunavyovipenda. ”