Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ni muhimu lakini pekee haitoshi:Guterres

Sindano imeandaliwa katika kituo cha umma  cha kampeni ya chanjo huko Sudani Kusini
UNMISS/Tim McKulka
Sindano imeandaliwa katika kituo cha umma cha kampeni ya chanjo huko Sudani Kusini

Chanjo ni muhimu lakini pekee haitoshi:Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameuambia mkutano wa kimataifa kuhusu chanjo  unaofanyika leo kupitia njia ya mtandao kwamba chanjo ni muhimu sana na imeokoa maisha ya mamilioni ya watu duniani lakini peke yake haitoshi kukabiliana na majanga makubwa ya kiafya kama linaloisumbua dunia hivi sasa la COVID-19.

Katika ujumbe wake kwenye mkutano huo ulioandaliwa na muungano wa chanjo duniani GAVI na mwenyejeji akiwa serikali ya Uingereza, Antonio Guterres amesema chanjo ni muujiza wa kuokoa Maisha na moja ya hatua muhimu za kihistoria za kunusuru afya ya umma duniani, kwani inaokoa maisha ya mamilioni ya watu kila mwaka.

Akitoa mfano amesema chanjo ilisaidia kutokomeza magonjwa kama ndui, inazuia magonjwa kama surau, rubella na pepopunda, lakini akaonya kwamba “Lakini pia tunakutana na wakati usiotabirika, COVID-19 ni mgogoro mkubwa kabisa wa afya ya umma katika kizazi chetu na kwa sasa hakuna chanjo, tunaposhirikiana kuisaka na kuitengeneza kuna somo moja muhimu tunapaswa kulielewa, kwamba chanjo peke yake haitoshi.”

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba dunia inahitaji mshikamano ili kuhakikisha kila mtu kila mahali ana fursa na kuongeza kuwa “Chanjo ya COVID-19lazima ionekane kama jambo jema kwa umma duniani, chanjo ya watu wote ambayo viongozi kadhaa duniani wanaitolea wito.”

 Hata hivyo ameonya kwamba “Watoto milioni 20 wanakosa kukamilisha chanjo zote na mtoto mmoja kati ya watano hapati chanjo kabisa. Na sasa katika kivuli hiki cha COVID-19 hali imekuwa mbaya zaidi, kwani kampeni za chanjo zinasitishwa. Pengo la kimataifa la utoaji chanjo huenda likaongezeka..”

 Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amewataka washiriki wa mkutano huo kuweka ahadi tatu, Mosi, kutafuta njia salama kuendelea kutoa chanjo hata wakati COVID-19 ikisambaa.

Pili , kutumia mitandao yote ya ufikishaji chanjo kufikisha huduma mbalimbaliza msingi za afya. Na tatu wakati chanjo ya COVID-19 itakapopatikana , kuhakikisha kwamba inamfikia kila mtu. 

Kwani amesema “Magonjwa hayaka mipakana ndio maana ufadhili kwa GAVI utakuwa muhimu sana kuhakikisha tunaendelea kupiga hatua kuelekea maendeleo endelevu.”