Baraza la Usalama lapitisha azimio kuhakikisha chanjo ya COVID-19 inafika kwenye mizozo

26 Februari 2021

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa amesema amefarijika na hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo kupiga kura na kupitisha azimio la kutaka pande zote katika mizozo kusitisha uhasama ili kutoa fursa ya kutoa chanjo  dhidi ya corona au Covid-19 na misaada mingine ya kibinadamu.

Dkt. Tedross Adhanom Ghebreyesus ameyasema hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao uliofanyika Geneva Uswis hii leo ambao ulijikita na usambazaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 kote duniani kupitia mkakati wa kimataifa wa chanjo unaosimamiwa na WHO ujulikanao kama COVAX.

Azimio hilo la Baraza la Usalama “Linazitaka pande zote katika migogoro ya silaha kujihusisha mara moja katika usitishaji uhasama wa muda mrefu na wa kudumu ili kuruhusu ufikishaji salama, usioingiliwa na usio na vizuizi wa chanjo za COVID-19 katika maeneo hayo ya vita vya silaha.”

Pia azimio hilo limeziomba nchi zilizoendelea kujitolea dozi za chanjo kwa nchi masikini na za kipato cha wastani na mataifa ,mengine yaliyo katika uhitaji hususan kupitia mkakati wa COVAX.

Mkakati huo unaoongozwa na Muungano wa chanjo duniani GAVI ambao unasaka na kupata chanjo kwa ajili ya nchi masikini, WHO, muungano wa kujiandaa na masuala ya magonjwa ya mlipuko na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF. Ombi hilo pia limeungwa mkono na Dkt. Tedros katika taarifa yake.

Mbali ya hayo azimio hilo pia l”imetoa wito wa kuimarisha mtazamo wa pamoja wa wa ushirikiano wa kitaifa na kimataifa ili kuwezesha fursa sawa za upatikanaji wa chanjo  dhidi ya COVID-19 na kwa gharama nafuu katika maeneo yaliyoghubikwa na vita vya silaha na maeneo yenye dharura za kibinadamu.”

Pia limesisitiza haja ya ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kuchapuza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa chanjo hizo.

Azimio hilo ambalo mswada wake uliwasilishwa kwenye Baraza hilo na Uingereza limepigiwa kura na kupitishwa bila kupingwa na wajumbe wote 15 wa Baraza la usalama.

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter