UNHCR inatoa tiba na ushauri nasaha kwa wakimbizi walioathirika na COVID-19 Colombia

1 Juni 2020

Nchini Colombia katika mpaka na Venezuela shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linashirikiana na wadau kutoka huduma za tiba na ushauri nasaha kwa mamia ya watu walioathirika na virusi vya Corona au COVID-19  na huduma zingine, wakiwemo wakimbizi wa Venezuela waliovuka mpaka kuja kusaka msaada.

Katika kituo cha afya cha Margarita mpakani mwa Venezuela na Colombia kina mama wakimbizi na wahamiaji lakini pia raia wa Colombia wakiwa na watoto wao wanasubiri huduma mbalimbali za afya miongoni mwao ni Damaris Pinate mama mkimbizi kutoka Venezuela ambaye amepata matumaini mapya ya maisha alipowasili katika kituo hiki cha afya

“Nina ujauzito wa miezi minne na sikuweza kufuatilia vipimo vya mimba yangu hadi nilipowasili hap na kupatiwa huduma. Madaktari wengi wamefunga milango yao kwa Wavenezuela. Bila kituo hiki kungekuwa na watu wengi sana ambao bado wangehitaji msaada.”

Kituo cha afya cha Margarta kilichopo katika eneo la Villa del Rosario Colombia kinatoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela lakini pia wenyeji wa Colombia ambao hawana fursa za huduma za afya na sasa kwa waathirika wa COVID-19

Kituo hiki kilijengwa na kinaendeshwa na UNHCR ikishirikiana na mashirika mengine ya kibinadamu na mamlaka za eneo hilo. Marcella Rosa ni mratibu wa kituo hiki

“Kituo hiki kina jukumu muhimu sana kwa sababu kinashughulikia moja kwa moja mahitaji ya kiafya ya eneo hili.”

UNHCR inasema dharura ya janga la corona imeziacha familia nyingi njiapanda mpakani bila njia yoyote ya kuweza kununua chakula au madawa.

Na mbali ya kukabiliana na COVID-19 kituo hiki kinawatibu wanawake wenye changamoto za ujauzito, wale wanaohitaji huduma za uzazi wa mpango na pia kinatoa msaada na ushauri masaha. 

Na sasa sababu ya COVID-19 UNHCR inaongeza msaada kwa kituo cha Margarita ili kiweze kukidhi mahitaji na watu wanaowasili kila siku kusaka huduma.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter