Skip to main content

Nyumba ya jirani ikiwaka moto, msaidie badala ya kujifungia mlango wako- Jolie

Akiwa Riohacha nchini Colombia, mjumbe maalum wa UNHCR, Angelina Jolie, amekutana na Ester Barboza mwenye umri wa miaka 17 ambaye amekuwa na ulemavu wa kutoona tangu akiwa na umri wa miaka mitatu na alikimbia Venezuela kutokana na ukosefu wa matibabu.
UNHCR/Andrew McConnell
Akiwa Riohacha nchini Colombia, mjumbe maalum wa UNHCR, Angelina Jolie, amekutana na Ester Barboza mwenye umri wa miaka 17 ambaye amekuwa na ulemavu wa kutoona tangu akiwa na umri wa miaka mitatu na alikimbia Venezuela kutokana na ukosefu wa matibabu.

Nyumba ya jirani ikiwaka moto, msaidie badala ya kujifungia mlango wako- Jolie

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati idadi ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela imefikia milioni 4, mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Angeline Jolie amesema kinachohijika hivi sasa ni utu na ubinadamu kuliko wakati wowote kwa watu ambao wana hofu ya kuwajibika kuonyesha uongozi katika kusaidia wakimbizi.

Bi. Jolie amesema hayo baada ya kutembelea Colombia na kushuhudia wimbi la wakimbizi wa Colombia wanaorejea nchini humo kutoka Venezuela sambamba na raia wa Venezuela wanaosaka hifadhi nchini humo kutokana na sababu za kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini mwao.

Kupitia taarifa iliyotolewa na UNHCR huko Geneva, Uswisi, mjumbe huyo maalum amesema “ni jambo la kipekee kuona Colombia, ambayo yenyewe inakabiliwa na changamoto nyingi, imeonesha utu kwa kusaidia wavenezuela wanaokimbia kwao. Napenda kutambua ujasiri wao, uthabiti na mnepo wa wananchi wa Colombia.”

Amesema zaidi ya wacolombia, 400,000 waliokuwa wamesaka hifadhi nchini Venezuela, sasa wamelazimika kurejea nyumbani kutokana na janga linaloendelea Venezuela, sambamba na wakimbizi milioni 1.3 wa Venezuela ambao wamesaka hifadhi Colombia.

Bi. Jolie amesema kama hiyo haitoshi, wavenezuela milioni 3.3 wanavuka mpaka na kuingia Colombia kusaka bidhaa na huduma za msingi akiongeza kuwa, “athari za uwepo wao kwenye huduma za umma Colombia zinatisha na kwamba baadhi ya hospitali za mpakani zinatoa huduma za dharura kwa wavenezuela sambamba na wacolombia.”

Alipotembelea eneo la Riohacha nchini Colombia, Mjumbe maalum wa UNHCR, Angelina Jolie alizungumza na Yoryanis Ojeda, mkimbizi wa zamani wa Colombia ambaye amerejea kutoka Venezuela kutokana na  uhaba wa chakula na tiba kwa watoot wake.
UNHCR/Andrew McConnell
Alipotembelea eneo la Riohacha nchini Colombia, Mjumbe maalum wa UNHCR, Angelina Jolie alizungumza na Yoryanis Ojeda, mkimbizi wa zamani wa Colombia ambaye amerejea kutoka Venezuela kutokana na uhaba wa chakula na tiba kwa watoot wake.

Amesema shule nazo zimechukua idadi ya wanafunzi maradufu kwenye madarasa na licha ya changamoto hizo,  “Colombia imeendelea kuacha mipaka yake wazi na inafanya kila iwezalo kupokea idadi kubwa ya wakimbizi hao waliokata tamaa.”

Ameongeza kuwa inachofanya Colombia ni uthibitisho wa kile kinachoendelea duniani ambako nchi zisizo na uwezo ndio zinafungua milango kwa walio na uhitaji, akiongeza kuwa “ombi la usaidizi wa kibinadamu lililotolewa na UNHCR na wadau kwa ajili ya wakimbizi wa Venezuela mwezi Disemba mwaka jana limefadhiliwa kwa asilimia 21 tu.”

Ni kwa mantiki hiyo, mjumbe huyo maalum ametaka hatua zaidi za usaidizi akisema “ninavyoondoka Colombia na katika miezi ijayo nitaajaribu kupeleka ujumbe wa watu kuacha hofu na kuonesha utu na ubinadamu.”

Amekumbusha kuwa nyumba ya jirani yako  ikiwa inawaka moto, unachotakiwa ni kusaidia na si kufunga mlango wako na kwamba, “uongozi ni kuwajibika kama ambavyo vizazi vilivyotutangulia viliwajibika kushughulikia vitisho vya amani na usalama na kujenga mfumo wenye kanuni duniani. Tunahitaji aina hiyo ya uongozi hivi sasa tena haraka,” amesema Bi. Jolie.

“Sitasahau kile nilichoona hapa, sitasahau wananchi wa Venezuela niliokutana nao hapa. Moyo wangu uko nao na ninatumaini nitarejea tena karibuni,” amesema mjumbe huyo maalum wa UNHCR.