Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nawakirimu si kwa kuwa nina uwezo bali kwa sababu ya upendo- Marta

Tarehe 24 Aprili 2019 mjini Cucuta Colombia mtoto akimkumbatia mama yake katika kituo cha wasamaria wema cha kupumzikia kwa watu wanaotembea ambao wataendelea na safari yao ya mguu kutoka Venezuela wakilenga kuingia Cali Colombia
UNICEF/Arcos
Tarehe 24 Aprili 2019 mjini Cucuta Colombia mtoto akimkumbatia mama yake katika kituo cha wasamaria wema cha kupumzikia kwa watu wanaotembea ambao wataendelea na safari yao ya mguu kutoka Venezuela wakilenga kuingia Cali Colombia

Nawakirimu si kwa kuwa nina uwezo bali kwa sababu ya upendo- Marta

Wahamiaji na Wakimbizi

Baadhi ya raia wa Colombia waliofungua milango ya nyumba zao ili kukirimu raia wa Venezuela wanaokimbia madhila nchini mwao wamesema kile wanachofanya si sadaka bali ni kitendo cha upendo na uwepo wa wakimbizi hao umebadili maisha yao

Kutana na Marta Duque, mcolombia mkazi wa Pamplona ambaye nyumba yake ameigeuza hosteli kwa ajili ya wavenezuela wanaomiminika nchini Colombia wakikimbia hali duni ya maisha nchini mwao.

Marta anasema siku moja usiku aliamua kuwasaidia wavenezuela baada ya kuwaona wamesongamana kwenye daraja moja mbele ya nyumba yake huku wakiwa wamenyeshewa mvua.

Anasema yeye na mumewe waliamua kugeuza gereji ya gari lao kuwa makazi ya wakimbizi hao wakiwapatia mikeka na blanketi.

Wakimbizi hao, wake kwa waume, vijana na watoto ambao wametembea kilometa 70 kutoka mpakani wanakirimiwa malazi na chakula bila gharama yoyote na kwa usiku mmoja idadi yao kwenye hosteli hii ya Marta ni takribani 100, Marta ambaye ametoa huduma hii kwa miaka miwili sasa anasema..

“Sebule yangu, eneo la kulia chakula na jiko vyote vimetoweka. Kuna watu wengi sana na hivyo lazima tutumie nyumba nzima kuhakikisha hakuna mwanamke au mtoto anasalia nje kwenye baridi. Hatuna siku ya mapumziko, mwaka mzima tunafanya kazi.”

Marta mwenyewe anahaha ili kuweza kukimu mahitaji yake lakini hilo halimzuii kusaidia wavenezuela akisema,,,

“Kile kilichonitia motisha zaidi ni kuona watoto, wengine wachanga zaidi na walio hatarini pamoja na wanawake ambao ndio kwanza wamejifungua, na wanawake wenye watoto njiti au wagonjwa. Hakuna mtu anawasaidia, hakuna mtu anawapatia chakula. Siwezi kuelewa. Watu wengi wana uwezo wa kusaidia lakini hawafanyi hivyo.”

Marta katika video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi anamalizia simulizi yake

Anasema haoni hicho afanyacho kuwa ni sadaka ya kipekee, bali anafanya kwa upendo na ana uhakika kwamba siku moja wakimbizi hao wasipokuwepo, atajisikia mpweke na kwamba hali hiyo ya kuwakirimu  imebadili maisha yake.