Pale amani inapoimarika na mkimbizi kuweza kujikwamua na kusaidia wakimbizi wenzake!

12 Oktoba 2018

Kurejea kwa amani nchini Colombia kumekuwa ni nuru kwa wavenezuela wanaokimbia nchi yao kutokana na ghasia na ukosefu wa huduma muhimu.

Hapa ni Las Delicias, Cucuta nchini Colombia, eneo linalopakana na Venezuela. Wanandoa wawili, Alvis na Marnellis wanaonekana wanatembea wakiwa wameshikana mikono, mwelekeo ni kwenye nyumba yao.

Nyumba hii waliijenga baada ya kukimbia maeneo ya ndani kabisa nchini mwao Colombia wakati wa mzozo wa wenyewe kwa wenyewe uliodumu miaka 50. Hivi sasa mzozo huo ni historia na hali si shwari nchi jirani ya Venezuela ambapo maelfu kwa maelfu ya raia wamefika kwenye mji huu na wanasaka hifadhi. Marnellis anasema ni kama ilivyokuwa simulizi yao akisema, “nasi pia tulikimbia kutokana na ghasia huko La Guajira na pindi tulipowasili kwenye mji huu, tulipitia  yale ambayo nao wanapitia. Nasi tulikuwa na njaa. Kwa hiyo tuliguswa sana tuliposhuhudia hali zao, na baada ya yote tuliyopitia, ambayo nao wanapitia, tukaona bora tuwasaidie.”

Marnellis na mumewe Alvis wamepatia hifadih wakimbizi 12 kutoka Venezuela. Wageni hawa hawalipi kodi yoyote bali wanasaidia kazi za nyumbani.

Graciela Sánchez naye ni raia wa Colombia ambaye aliwahi kuwa mkimbizi na sasa amepatia hifadhi wakimbizi 18 kutoka Venezuela na miongoni mwao ni Janire ambaye anasema“anatupatia msaada wa kimawazo kwa sababu sisi ni marafiki tu na si sehemu ya familia  yake.”

Kwa ujumla katika mji wa Las Delicias, familia 23 zinahifadhi jumla ya wakimbizi wageni 130 ambapo idadi kubwa ya wenyeweji wenyewe walikuwa wakimbizi wa ndani.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR linasaidia kulipa gharama za maji na umeme.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud