Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 inaongeza madhila ya kibinadamu Yemen:OCHA

Madaktari katika kituo cha Karantini cha Aden Yemen wamepokea vifaa vya kujikinga kutoka kwa UNICEF
© UNICEF
Madaktari katika kituo cha Karantini cha Aden Yemen wamepokea vifaa vya kujikinga kutoka kwa UNICEF

COVID-19 inaongeza madhila ya kibinadamu Yemen:OCHA

Afya

Yemen nchi iliyoathirika vibaya na vita vya wenyewe kwa wewe sasa imeachwa ikabiliane na janga la virusi vya corona au COVID-19 na mfumo wa afya ambao umesambaratika na bila usaidizi zaidi wa kifedha limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA.

Wataalam wa magonjwa wanakadiria kwamba virusi vya corona vitasambaa haraka na katika sehemu kubwa huku vikiwa na athari mbaya sana kwa taifa hilo masikini na lenye watu walio katika hatari zaidi kuliko nchi nyingi duniani.

 Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa OCHA Jens Larke amesema “Yemen iko njiapanfda hivi sasa, hali inatisha, wanazungumzia mfumo wa afya kusambaratika, wanazungumzia kuwarudisha watu kwa sababu hawana mashine za kutosha za hewa ya Okisijeni. Hsawana vifaa vya kutosha vya kujikinga na corona PPE, na kwamba idadi ya rasmi inayoripotiwa na wagonjwa ni muhimu sana kama nilivyosema tunafanyakazi kwa makisio kwamba kuna maambukizi mengi katika jamii ambayo yanaendelea.”

Ikiwa ni nusu tu ya vituo vya afya Yemen ndio vinavyofanyakazi OCHA inasema ufadhili kwa ajili ya operesheni za nchi hiyo ni muhimu huku zikiwa zinahitajika dola bilioni 2 hadi kufikia mwisho wa mwaka huu.

Changamoto za kifedha

Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia wataendesha mkutano wa ahadi za ufadhili kwa njia ya mtandao mnamo Juni 2 ili kuchangisha fedha kwa ajili ya nchi hiyo.

“Tunaelekea katika wakati mbaya na tusipo pata fedha program ambazo zinawasaidia kufanya watu waendelee kuishi na ni muhimu sana katika kupambana na COVID-19, itabidi tuzifunge. Na dunia itashuhudia nini kitakachotokea katika nchi ambayo haina mfumo wa afya unaofanya kazi kupambana na COVID-19 na sidhani kuna yeyote anayetaka kuliona hilo.”

Zaidi ya operesheni 30 za Umoja wa Mataifa ziko katika hatari ya kufungwa katika wiki zijazo kutokana na ukata wa ufadhili. Timu za kupambana na COVID-19 zimefadhiliwa tu hadi katika wiki sita zijazo.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO takwimu mpya zinaonyesha kwamba Yemen ina wagonjwa 184 na vifo 30 vya corona. Hata hivyo “idadi kamili huenda ni kubwa Zaidi kwani kuna upungufu katika upimaji, mashirika ya misaada Yemen yanafanya kazi kwa misingi kwamba maambukizi ya kijamii yanafanyika nchi nzima na kwamba ni nus utu ya mvituo vya afya nchini humo ndio vinafanyakazi. Mfumo wa afya wa Yemen unahitaji msaada mkubwa ili kuweza kukabiliana na tishio la COVID-19. Mashirika ya misaada ya kibinadamu uyanaongeza kasi ya msaada kuwafikia wengi, ili kuzuia na kudhibiti maambukizi.”

 Msaada uliokwisha wasili

 Hadi kufikia sasa tani 125 za msaada zimewasili huku tani zingine 6,600 za vifaa vya kupima, vifaa binafsi vya kujikinga (PPE) na vifaa kama mashine za vyumba vya wagonjwa mahututi vikitarajiwa kuwasili hivi karibuni.

OCHA inasema mashine za Oksijeni na vifaa binafsi vya kujininga vinahitajika haraka . Pia kulinda mipango ya muda mrefu ya afya nchini humo kama vile maji na usafi, lishe na sekta zingine ambazo zinatoa huduma muhimu ya kujikinga na maambukizi kwa mamilioni ya watu wa Yemen.

Kwa mujibu wa msemaji wa OCHa Jens Laerke jana ndege ya Umoja wa Mataifa iliwasili katika mji wa Aden nchini Yemen ikiwa na wafanyakazi wa kimataifa.”Wafanyakazi wenzetu wa ndani nan je wanashirikiana kwa Pamoja kufikisha program muhimu ikiwemo baadhi ya wafanyakazi wa kimataifa ambao wanafanyakazi wakiwa sehemu mbalimbali Pamoja na wafanyakazi walio salia Yemen na wale wa kitaifa.Kwa sasa wafanyakazi wa kitaifa wa Yemen ndio sehemu kubwa ya wafanyakazi wa misaada nchini humo.”

 Vita nchini Yemen vimekuwa vikiendelea tangu mwaka 2014 wakati Wahouthi waliposhika udhibiti eneo la Kaskazini mwa Yemen na kushikilia mji mkuu Sa’naa na kuilazimisha serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kukimbilia mjini Aden.  

Na tangu mwaka 2015 muungano wan chi nyingi za Kiarabu unaoongozwa na Saudia umekuwa ukipambana na waasi wa Houthi ili kuirejesha serikali halali ya Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi madarakani, hali ambayo imesababisha mgogoro mkubwa kabisa wa kibinadamu ukiwaacha mamilioni ya watu katika janga la uhaba wa chakula na huduma za afya.