MachafukoYemen yasababisha misaada kusitishwa: OCHA

4 Disemba 2017

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA nchini Yemen, Jamie McGoldrick  ameomba kusitishwa kwa utoaji wa huduma za kibinadamu nchini humo baada ya mashambulizi ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengi katika mji mkuu Sanaa.

Bwana McGoldrick amesema hali ya usalama kwa watoa huduma wa mashirika tofauti ni   hatarishi  kutokana na migogoro ya hivi karibuni.

Amesema mitaa ya  mji wa Sanaa ni sawa na uwanja wa vita , wananchi wamekwama majumbani , hivyo uwezo  wa kuwafikishia   misaada na huduma ni mdogo  na hatarishi.

Aidha amesema watoa huduma wanazidi kupokea simu za uhitaji kutoka kwa maelfu ya wananchi wenye  uhitaji wa  vitu mbalimbali ikiwemo dawa, chakula, maji, mafuta ya taa, ila watoa huduma wanashindwa kufanya hivyo kwa kuhofia usalama wao.

Mkuu huyo wa OCHA nchini Yemen anatoa wito kwa pande zote kinzani  na pia nchi wanachama wenye nafasi ya kusaidia kusitisha mapigano, ili mashirika ya kibinadamu yaweze kuwafikia wananchi walio katika hali ya uhitaji mkubwa ambao asilimia kubwa ni wanawake watoto na wazee wasiojiweza.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter