Msaada waliotupatia UNFPA umetusaidia kuendeleza huduma za wakunga-Wakunga Tanzania

5 Mei 2020

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya wauguzi na wakunga , Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la afya WHO umesema mchango wa wahudumu hao wa afya hauna kipimo hasa wakati huu ambao janga la virusi vya corona au COVID-19 linaitikisa dunia na wao wako msitari wa mbele kupambana nalo. Kaulimbiu ya mwaka huu ni "waunge mkono wauguzi na wakunga".

Nchini Tanzania Chama Cha wakunga TAMA, kimeushukuru Umoja wa Mataifa kupitia shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA kwa kuunga mkono harakati na juhudi za wakunga kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa uzazi. Rais wa TAMA, Mkunga mbobevu wa miaka mingi, Bi Feddy Mwanga anaanza kwa kueleza kazi kubwa ya chama cha wakunga.
 “Kazi kubwa ya Chama cha wakunga Tanzania (TAMA) ni kuelimisha wakunga ili kuwapa stadi stahiki za kuokoa mama na mtoto pale wanapopata matatizo wakati wa ujauzito, kujifungua, mara baada ya kujifungua  na kumhudumia mtoto mchanga. Ili tuweze kufanya mafunzo haya tumepata msaada wa kifedha na vifaa kutoka kwa mashirika mbalimbali. Nitambue msaada mkubwa kabisa ambao tumeupata kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa  la idadi ya watu duniani, UNFPA ambao wamekuwa mstari wa mbele wa kutupa msaada wa kifedha na vifaa vya mafunzo lakini pia wametupa msaada mkubwa wa samani  yaani furniture katika ofisi yetu ya makao makuu. Msaada huu umetupa utulivu wakati wa kufanya kazi hasa kwa wakati huu wa janga la virusi vya corona tunaweza kufanya kazi kwa nafasi inayotosheleza ya mtu hadi mtu.”

Bi Mwanga anasema kwa kuzingatia kuwa mkunga mtaalamu ana uwezo  wa kutoa huduma hadi asilimia 87 ya kuzuia  vifo vitokanavyo na uzazi, wameendelea kutoa huduma hata wakati huu wa changamoto ya COVID-19

“Wakunga tumeendelea kutoa huduma yetu na tumeendelea kuhakikisha kwamba wakina mama wanajifungua salama na  kama tunavyoona vifo vitokanazo na uzazi vinapungua japo sio sana lakini vinapungua. Tumefanya uhamasishaji mkubwa  katika jamii kuhakikisha akina mama wanajifungulia katika vituo vya afya ambapo wanapata  huduma ya matibabu ya kitaalum.Tunafurahia sana kwamba Idada ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kwa kiwango cha kuridhisha kabisa.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter