Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wauguzi na wakunga milioni 9 watahitajika kukidhi mahitaji ya afya duniani:WHO

Mkunga Adelaide Raul kutoka Msumbiji akifurahi na mama baada ya kumzalisha watoto mapacha
UNFPA Mozambique
Mkunga Adelaide Raul kutoka Msumbiji akifurahi na mama baada ya kumzalisha watoto mapacha

Wauguzi na wakunga milioni 9 watahitajika kukidhi mahitaji ya afya duniani:WHO

Afya

Dunia itahitaji ongezeko la wauguzi na wakunga milioni 9 ili kutimiza ahadi ya kutoa fursa ya huduma za afya kwa wote ifikapo mwaka 2030 limeonya leo shirika la afya ulimwenguni WHO.

Kwa mantiki hiyo WHO na wadau watautumia mwaka huu wa 2020 kupigia upatu uwekezaji katika wahudumu hao muhimu wa afya. Akihimiza kuhusu hilo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhamon Ghebreyesus amesema “wauguzi na wakunga ni uti wa mgongo wa kila mfumo wa afya na mwaka 2020 tunatoa wito kwa nchi zote kuwekeza kwa wauguzi na wakunga kama sehemu ya ahadi ya huduma za afya kwa wote.”

Ameongeza kuwa mwaka 2020 ni “Mwaka wa wauguzi na wakunga” n ani maadhimisho ya miaka milenia tangu kuzaliwa kwa Florence Nightngale muasisi wa uuguzi.

Nesi akijaza chanjo katika bomba la sindano
UNICEF/UN066747/Rich
Nesi akijaza chanjo katika bomba la sindano

Mwaka huu ni wq kusherehekea wanataaluma ambao wanatoa huduma mbalimbali muhimu kwa watu kila mahali. Mbali ya kuzuia, kubaini, kupima magonjwa na kutoa huduma ya kitaalam wakati wa kujifungua wauguzi na wakunga pia wanaokoa Maisha ya watu katika majanga na dharura za kibinadamu na vita.

Hivi sasa kote duniani kuna wauguzi milioni 22 na wakunga milioni 2 wakiwa ni nusu ya wafanyakazi wote wa huduma za afya kwa mujibu wa WHO.
Hata hivyo shirika hilo limesema dunia inahitaji wahudumu wafaya milioni 18 zaidi na takribani nuu yao ni wauguzi na wakunga ili kuweza kutimiza lengo la huduma za afya kwa wote kabla ya kumalizika muongo huu kwenda sanjari na ahadi iliyowekwa na viongoziwa dunia kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka jana.

Mwanasesere anayetumika kwa mafunzo na wakunga nchini Uganda.
UNFPA
Mwanasesere anayetumika kwa mafunzo na wakunga nchini Uganda.

Kwa mwaka huuWHO itashinikiza hatua za kuhakikisha kwamba wauguzi na wakunga wanaweza kufanya kazi kufikia kilele cha uwezo wao.
WHO inasema maeneo ambayo ni muhimu kwa uwekezaji ni pamoja na kuajiri wauguzi na wakunga wenye utaalam, kuwafanya wauguzi na wakunga kuwa kitovu cha huduma za afya za msingi na kuwasaidia katika kuchagiza afya bora na kuzuia magonjwa.